Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, kwa mara nyingine serikali ya Ujerumani imefeli katika juhudi zake za kutafuta gesi ya kufidia ile ya Russia. Huko nyuma vyombo hivyo vya habari viliripoti kufeli Ujerumani kununua gesi ya Qatar na sasa hivi vimeripoti kufeli tena baada ya kushindwa kuingiza nchini humo gesi kutoka Canada.
Jana Jumatano shirika la habari la FARS lililinukuu gazeti la Die Zeit la Ujerumani likitangaza kufeli juhudi za kansela wa nchi hiyo, Olaf Scholz, kuingiza gesi kutoka Canada. Kansela huyo wa Ujerumani amekuwa akifanya juhudi za usiku na mchana ili kuwapunguzia makali ya kukosa gesi wananchi wa nchi hiyo, lakini hadi sasa ameshindwa kupata gesi ya kufidia ile ya Russia.
Jumatatu wiki hii, Scholz alionana na waziri mkuu wa Canada, Justin Trudeau na kumuomba aipatie Ujerumani japo gesi kidogo kupitia Bahari ya Atlas. Lakini inaonekana Trudeau amekataa ombi hilo la kubembeleza la kansela wa Ujerumani.
Waziri Mkuu wa Canada ametumia lugha ya ujanja kukataa kuzipa nchi za Ulaya gesi yake ambazo zimelemewa na balaa la kukosa nishati kutoka kwa Russia. Trudeau amesema, hadi sasa hakuna mradi wowote wa wazi wa kibiashara wa kujenga suhula za kuhamishia gesi asilia ya eneo la Saint John huko Canada (LNG) kwenda nje ya nchi hiyo.
Waziri Mkuu wa Canada pia amesema, si kazi nyepesi hata kidogo kuweza gesi asilia ya Canada kufikishwa katika nchi za Ulaya kwani inabidi kwanza kujengwe bomba refu kutoka magharibi mwa Canada hadi kwenye kituo maalumu cha kuhifadhi gesi hiyo katika Bahari ya Atlas ambacho nacho pia hakijajengwa hivi sasa.
Amesema, ujenzi wa bomba hilo na kituo hicho unahitaji uwezekezaji wa fedha nyingi na muda mrefu hasa kutokana na kuweko pia wajibu wa kulindwa mazingira.