Lebanon yapongeza misaada, uungaji mkono wa Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon, Abdullah Bou Habib amesifu na kupongeza misaada na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa taifa hilo la Kiarabu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Beirut Ijumaa akiwa pamoja na Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abdullah Bou Habib amesema Lebanon inakaribisha na kuunga mkono suala la kupanuliwa uhusiano wa pande mbili wa nchi yake na Iran.

Kabla ya kikao hicho na waandishi wa habari, mawaziri hao walifanya mazungumzo na kujadili uhusiano wa pande mbili wa Iran na Lebanon, na vile vile masuala ibuka ya kieneo na kimataifa.

Kwa upande wake, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuwa rafiki ya Lebanon hata katika vipindi vigumu.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameashiria mgogoro wa nishati nchini Lebanon na kueleza kuwa, “Ujumbe wa Lebaon uliitembelea Iran karibuni kujadili namna ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nishati (wa Lebanon), tupo tayari kutoa msaada wa aina yoyote.”

Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepongeza hatua zilizopigwa katika utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya mataifa haya mawili, alipoitembelea Lebanon mnamo Oktoba mwaka 2021.

Adbdollahian ameongeza kuwa, Iran ambayo ina teknolojia ya hali ya juu, ipo tayari kuunda na kukarabati vituo vya nishati katika nchi hiyo ya Kiarabu. Kadhalika ameeleza bayana kuwa, Iran itaendelea kuunga mkono harakati za muqawama za Lebanon na Palestina, na kwamba Jamhuri ya Kiislamu inautazama usalama wa Lebanon kama usalama wake mwenyewe na eneo zima la Asia Magharibi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *