LHRC: Wafungwa na walio nje Tanzania waruhusiwe kushiriki uchaguzi

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) kimeibua kile kilichoyaita kuwa mapungufu katika miswada ya sheria ya uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa.

Katika mapendekezo yake, kituo hicho kinataka sheria za uchaguzi zijumuishe wafungwa kupiga kura katika uchaguzi wa rais na wabunge huku kikisisitiza kupatikana kwa katiba mpya.

Muswada wa sheria ya tume ya taifa ya uchaguzi, muswada wa sheria ya uchaguzi wa rais na wabunge na muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa iliwasilishwa Novemba 10 bungeni na kufungua pazia pana la mabadiliko katika chaguzi za kisiasa nchini Tanzania.

Hata hivyo tangu kufunguliwa kwa pazia hilo, wadau mbalimbali wa kisiasa na utawala bora, wamekuwa wakitoa maoni yao, baadhi wakipongeza na wengine wakitaka maboresho ili sheria hizo zikidhi chaguzi huru na za haki.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) kimefanya uchambuzi wa miswada hiyo kabla ya kuwa sheria kamili na kubaini mapungufu kadhaa, ikiwamo wakurugenzi wa halmashauri za wilaya kuwa wasimamizi wa uchaguzi, watumishi wa umma kuwa sehemu ya tume ya uchaguzi na tume kuendelea kutegemea bajeti ya serikali.

Kadhalika, kituo hicho kilipendekeza muswada wa sheria ya uchaguzi kutoa haki kwa jumuiya ya Watanzania waishio nje ya nchi, kupata haki ya kupiga kura. Pamoja na hayo wakasisitiza wakisema katiba mpya ndiyo suluhisho la kudumu la demokrasia Tanzania.

Pamoja na LHRC wachambuzi wengine wa siasa, wamechambua miswada hii na kupongeza lakini wakiitaka serikali kutilia mkazo suala la katiba mpya na wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu basi suala la tume huru ya uchaguzi lisifanyiwe mzaha.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *