Lissu arejea nyumbani kwa kishindo; ujio wake utahuisha upinzani Tanzania?

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu amerejea nyumbani kutoka uhamishoni baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuondoa marufuku ya mikutano ya kisiasa ya hadhara.

Lissu amewasili leo Jumatano katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akitokea Ubelgiji, na kupokea viongozi, wanachama na mamia ya wafuasi wa Chama cha upinzani cha Chadema.

Jeshi la polisi limeimarisha ulinzi na kuhakikisha wafuasi hao hawaingii ndani ya eneo la uwanja na badala yake wanabaki nje ya lango kuu pembezoni mwa barabara ya Nyerere.

Shamra zilitawala nje ya lango kuu la kuingia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijijini Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya Lissu kuwasili.

Wakizungumza na gazeti la Mwananchi, wafuasi hao wamesema wana furaha tele kwa kurejea nyumani kwa kiongozi huyo, kwani wanaamini ataleta mabadiliko kwenye siasa za Tanzania. Lissu, ambaye alipigwa risasi 16 katika jaribio la kutaka kumuua mwaka 2017 akiwa ndani ya gari lake jijini Dodoma, amekuwa akiishi uhamishano nchini Ubelgiji tokea wakati huo.

Anarejea nchini Tanzania kufuatia tangazo la Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni kwamba, marufuku ya mikutano ya kisiasa iliyowekwa na mtangulizi wake hayati John Magufuli imeondolewa.

Amesema anarejea Tanzania kwa ajili ya mwanzo mpya, kwani Rais Samia Suluhu Hassan kupitia serikali yake na chama chake wameonyesha wako tayari kwa safari mpya.

Tundu Lissu alisifika kwa ukosoaji wake dhidi ya serikali ya hayati Magufuli. Hata kabla ya hapo tayari alikuwa ni mwanasiasa maarufu, na kurejea kwake kunatazamiwa kuupa msukumo mpya na kuupiga jeki upinzani nchini humo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *