Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Maseno alipigwa risasi jana Jumatatu na kuuawa wakati wa maandamano ya kupinga serikali yaliyoongozwa na Azimio la Umoja One Kenya.
William Mayange, ambaye alipigwa risasi shingoni baada ya waandamanaji kuvamia kituo cha polisi cha Maseno, alitangazwa kufariki dunia alipofikishwa katika Hospitali ya Coptic.
Polisi wamesema waandamanaji, ambao ni pamoja na wanafunzi, walivamia safu ya polisi ya Maseno wakati wa maandamano, na kusababisha maafisa hao kutumia risasi za moto kuwatawanya vijana hao.
Ripoti ya polisi imedai kuwa wanafunzi hao waliharibu takriban nyumba 10 katika kituo cha Polisi cha Maseno.
Awali Rais William Ruto wa Kenya alikuwa amesema kwamba hatakubali “kutoijali nchi” baada ya maandamano ya ghasia kuikumba miji kadhaa ya nchi hiyo.
“Nitahakikisha kama rais kwamba nchi hii inaongozwa na sheria, na hakuna chochote zaidi ya sheria na katiba kitakachokuwa sehemu ya kile tunachofanya,” Bw Ruto alisema.
Ruto amemtuhumu kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwa anajaribu kuanzisha mgogoro kwa mara ya pili, nchini Kenya kama ule wa baada ya uchaguzi wa 2017 uliomlazimisha Rais wa wakati huo, Uhuru Kenyatta, kufikia makubaliano ambayo yalimpa mapendeleo ya serikali.