Maandamano ya kupinga safari ya waziri wa vita wa Israel nchini Morocco yamesambaa zaidi katika miji mbalimbali ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Faraan: Wananchi wa Morocco katika miji mbalimbali ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu, Rabat, wamefanya maandamano wakipinga safari ilioyofanywa nchini humo na waziri wa vita wa utawala haramu wa Israel, Benny Gantz, nchini Morocco na wametoa wito wa kusitishwa mwenendo wa kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel.
Waandamanaji hao pia wametangaza mshikamano na uungaji mkono wao kwa wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.
Maandamano hayo yameitishwa na harakati ya kuwatetea Wapalestina na kukabiliana na mwenendo wa kuanzishwa uhusiano na Israel ya Morocco. Kabla ya hapo wananchi wa Morocco na mashirika yasiyo ya kiserikali na waungaji mkono wa wananchi wa Palestina nchini Morocco walieleza hasira zao kutokana na ziara ya hivi karibuni ya waziri wa vita wa Israel nchini humo na kulaani hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel.
Sekretarieti ya Kongamano la Waarabu la Morocco imelaani ziara ya hivi karibuni ya waziri wa vita wa Israel nchini Morocco na kutiwa saini hati ya maelewano kati ya pande hizo mbili, na imeitaja hatua hiyo kuwa ni kudharau matakwa ya watu wa Morocco na kuvunjia heshima damu ya maelfu ya Wamorocco waliosabilia roho zao katika historia kwa ajili ya Palestina, Quds na matukufu ya Kiislamu.
Morocco ilikuwa nchi ya nne ya Kiarabu baada ya Imarati, Bahrain na Sudan kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni mwaka hapo 2020. Suala hilo limepingwa vikali na Ulimwengu wa Kiislamu.