Maandamano ya kupinga Uzayuni yafanyika nchini Sweden na Italia

Wapinzani wa jinai za utawala wa Kizayuni katika mauaji ya kimbari ya wananchi madhulumu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza wamefanya maandamano makubwa nchini Sweden na Italia wakitaka kukomeshwa mara moja mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi wa Palestina.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anatolia, waandamanaji wanaopinga jinai za utawala wa Kizayuni katika maandamano yaliyofanyika siku ya Jumamosi huko Stockholm, mji mkuu wa Sweden, wakiwa na mabango yenye maandishi yaliyosomeka, “sitisha mauaji ya kimbari” na “watoto wanauawa Gaza”, wamelaani jinai za utawala wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.

Maelfu ya waungaji mkono wa Palestina pia wamefanya maandamano makubwa katikati mwa Roma, mji mkuu wa Italia wakisisitiza ulazima wa kukomeshwa mauaji ya kimbari ya wananchi wa Palestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni.

Huku wakiwa wamebeba bendera za Palestina na mabango yaliyoandikwa maneno yanayosema, “simamisha mauaji ya kimbari” wamepiga nara zinazosema: “Ikomboeni Palestina” na “Netanyahu ni muuaji.”

Kwa kupita siku 351 tangu kuanza vita vya Gaza, utawala wa Kizayuni bado haujafikia malengo yake katika vita hivyo, yaani ya kuangamizwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na kukombolewa mateka wa Kizayuni.

Wizara ya Afya ya Palestina ilitangaza siku ya Ijumaa kuwa tangu tarehe 7 Oktoba wakati utawala wa Kizayuni ulipoanza mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza, Wapalestina 41,391 wameuawa shahidi na wengine 95,760 wamejeruhiwa katika mauaji ya umati yanayofanywa na utawala huo katika ukanda huo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *