Makumi ya maelfu ya wakazi wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina (Israel) wameandamana kulalamikia maamuzi yaliyochukuliwa na serikali ya Benjamin Netanyahu ya kubana mfumo wa mahakama wa utawala huo.
Maandamano ambayo yamefanyika karibuni katika miji ya Tel Aviv na Haifa yamewashirikisha watu wengi zaidi ikilinganishwa na yale yaliyofanyika katika miji mingine ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Yariv Levin, Waziri wa Sheria katika baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu hivi karibuni aliwasilisha mpango kwa ajili ya kufanyia mabadiliko mfumo wa mahakama wa utawala wa Kizayuni; ambapo lengo ni kubana shughuli za mamlaka ya mfumo wa mahakama wa utawala huo.
Mpango huo unabana mamlaka ya Mahakama Kuu katika nyanja mbili. Kwa upande mmoja ni kuwa, baraza la mawaziri litakuwa na mamlaka kamili ya kuwateuwa majaji ikiwa ni pamoja na Jaji wa Mahakama Makuu ya utawala huo wa Kizayuni. Katika upande wa pili, mpango huo unabana pakubwa uwezo wa Mahakama Kuu wa kufuta sheria na maamuzi ya serikali na badala yake kutoa mamlaka kwa Knesset (Bunge la utawala wa Kizayuni) kutunga upya sheria ambazo mahakama itakubali zifute kwa kuidhinishwa na wabunge 61. Kwa hiyo, mpango huo unavuruga kanuni ya mgawanyo wa madaraka na kuliongezea uzito bunge na baraza la mawaziri mkabala wa muundo wa mahakama.
Wakati huo huo mpango huo uliowasilishwa na baraza la mawaziri la Netanyahu mbali na kudhoofisha muundo wa mahakama wa utawala wa Kizayuni kwa iana fulani unatoa mwanya wa kupewa kinga viongozi ambao wana kesi katika vyombo vya mahakama vya utawala huo. Katika baraza la sasa la Mawaziri la Netanyahu, yeye mwenyewe na pia baadhi ya mawaziri wake wanakabiliwa na kesi mbalimbali za ufisadi na pia ugaidi. Wakati huo huo wanaokosoa mpango huo wanaamini kuwa, Netanyahu na baadhi ya mawaziri wake wanafanya kila wawezalo kuudhofisha muundo wa sasa wa mahakama ili kufunga mafaili ya kesi zinazowakabili. Wapinzani wanasema kuwa mpango huo utahitimisha uhuru wa idara ya mahakama ya Israel na kulifanya suala la kuzuia na kupambana na ufisadi kuwa gumu katika ardhi hizo za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Nukta nyingine ni hii kuwa, waandamanaji na wakosoaji wanaamini kuwa mpango huo wa utawala wa Kizayuni unaelekea upande wa mfumo wa udikteta na kwamba demokrasia inayoshuhudiwa katika utawala huo itasambaratishwa kikamilifu. Ripota wa shirika la habari la Ufaransa ameandika kuhusiana na hilo kwamba, waandamanaji huko Israel wamebeba mabango yenye maandishi kama “serikali ya fedheha”, “tunataka kung’olewa dikteta” na “Benjamini Netanyahu hataki demokrasia na sisi hatuhitaji mafashisti.”
Suala jingine muhimu ni kwamba kufanyika maandamano makubwa katika miji mikubwa ya utawala wa Israel kama vile Tel Aviv na Haifa kunathibitisha wazi kuwa baraza jipya la Netanyahu limekabiliwa na maandamano makubwa ya mapema; maandamano ambayo yanawashirikisha wapinzani wake wa kisiasa na pia kujumuisha idadi kubwa zaidi ya waandamanaji kwenye miji muhimu ya utawala huo. Maudhui hii inathibitisha kwamba baraza hilo jipya linakabiliwa na mashinikizo makali na kwamba hali ya usalama na kisiasa katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ni tata mno.
Ehud Barak, waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Tel Aviv ameandika katika makala iliyochapishwa karibuni katika gazeti la Kiibrania la Yedioth Ahronoth kwamba: Hitilafu zilizopo na serikali ya Netanyahu zimefikia kiwango cha vita na hiyo ni indhari ya wazi. Hii ni kwa sababu hatari inakaribia na bila shaka itasambaratisha mfumo wa kisiasa ambao umejengeka juu ya msingi wa kughusubu ardhi za wengine. Matukio mabaya yataendelea kufuatia kuanguka kwa Waisraeli. Kwa hiyo wanapasa kufungua macho yao na kujiuliza wanasimama wapi kwenye mapambano haya, na kisha kujipatia jibu halisi bila kujali litakuwa chungu na zito kiasi gani.