Moja ya matukio muhimu yaliyojiri katika Siku ya Nakba mwaka huu ni maandamano yaliyofanywa na Wazayuni wanaopinga vita dhidi ya Gaza. Wazayuni hao waliandamana mbele ya jengo la Wizara ya Vita ya Israel huko Tel Aviv.
Jana tarehe 15 Mei ilisadifiana na kumbukumbu ya maadhimisho ya miaka 76 ya Nakba. Kila mwaka, tarehe 14 na 15 mwezi Mei Wazayuni huadhimisha kumbukumbu ya kuasisiwa utawala bandia wa Israel. Hata hivyo mwaka huu umekuwa tofauti na miaka iliyopita. Mwezi wa 8 unapita sasa tangu utawala wa Kizayuni wa Israel uanzishe vita dhidi ya watu wa Gaza. Moja ya malengo makuu ya utawala wa Kizayuni ya kuendeleza vita na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza ni eti kuwakomboa mateka wake ambao wanashikiliwa na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas). Hata hivyo, lengo hilo halijafikiwa hadi sasa, na baraza la mawaziri la Israel, badala ya kuzungumza na kujadiliana na Hamas ili kufanikisha kuachiwa huru mateka hao, linaendelea kusisitiza vita; suala ambalo kivitendo limeibua maandamano ya Wazayuni dhidi ya baraza la mawaziri la Netanyahu.
Katika siku za hivi karibuni, walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakiandamana kupinga na kulalamikia sera za Benjamin Netanyahu na kushindwa kwake kufikiwa mapatano ya kuachiwa huru mateka wa utawala wa kizayuni wanaoshikiliwa Ukanda wa Gaza. Walowezi wa Kizayuni wanaondamana katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) wanataka kuondoka madarakani baraza la mawaziri la Netanyahu na kufanyika uchaguzi wa mapema. Katika maandamano hayo, Wazayuni wametoa nara mbalimbali na kutaka kutiwa saini mapatano ya kubadilishana mateka na harakati ya Hamas.
Juzi pia Wazayuni wanaounga mkono mapatano ya kubadilishana mateka na wanamapambano wa Palestina huko Gaza, kwa mara nyingine waliandamana mbele ya Wizara ya Vita ya Israel mjini Tel Aviv. Aidha imeelezwa kuwa waandamanaji hao pia waliwasha moto mbele ya jengo la Wizara ya Vita ya Israel. Baada ya miezi saba na licha ya madai na nara zote kuhusu kuangamiza Hamas, Israel bado inaendelea na vita vikubwa na Hamas. Akiwa waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Netanyahu yuko tayari kusabilia kila kitu kwa ajili ya maslahi yake binafsi.
Ni wazi kuwa, hakuna matumaini yoyote ya kuinusuru Israel katika kinamasi ilichotumbukia ndani yake kutokana na hali sasa. Hii leo, Israel iko katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miakka 76; na hii ndiyo sababu kuu ya maandamano makubwa yanayofanyika dhidi ya baraza lake la mawaziri hata katika kusherehekea kumbukumbu ya kuasisiwa utawala huo (Siku ya Nakba).
Ali Abdi, mchambuzi wa masuala ya Palestina, anaamini kuwa maadhimisho ya Siku ya Nakba mwaka huu yamefanyika katika hali ambayo utawala wa Kizayuni, pamoja na kushindwa pakubwa kijeshi, kijasusi na kisiasa katika operesheni ya kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa na makundi ya muqawama ya Palestina, unakabiliwa na maandamano ya dunia nzima, jamii iliyogawanyika na migogoro ya ndai ambayo haijawahi kushuhudiwa katika historia ya utawala huo.