Mabilioni yanavyoteketea kwenye kampeni za Kenya

Nairobi/Kenya. Wanasiasa wanazidi kumwaga mabilioni ya fedha katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, huku mamilioni ya wapigakura wakihangaika kutokana na makali ya njaa na bei za juu za bidhaa, Gazeti la Taifa Leo linaripoti.

Hali ikiwa hivyo, kumeripotiwa idadi ya watu ambao wanahitaji chakula kwa dharura inaongezeka kila uchao nchini humo, hasa katika maeneo ya kaskazini mashariki, pwani na bonde la ufa.

Kwa sasa pakiti ya kilo mbili ya unga wa mahindi inauzwa kwa Sh220 madukani (Sh4,340 za Tanzania). Bei ya bidhaa nyinginezo pia imeongezeka maradufu ikilinganishwa na mwaka jana.

Wananchi wanapoendelea kuumia, wanasiasa nao wamekuwa wakilaumiana kuhusu bei ya vyakula kupaa, ambapo wale wa Kenya Kwanza (timu ya William Ruto) wanadai kuwa Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta wameshirikiana kupandisha bei ya bidhaa nchini, ukiwemo unga.

Lakini wanasiasa wa Azimio la Umoja (timu Raila), wanamlaumu Dk Ruto kwa kushindwa kuchukua hatua kupunguza bei ya bidhaa kwa kuwa naye angali serikalini.

Kwa upande wake Rais Kenyatta, amekuwa akijitetea kuhusu bei za bidhaa akidai hali hiyo imesababishwa kwa kiasi kikubwa na vita nchini Ukraine.

Hata hivyo, wataalamu wanalaumu sera za utawala wa Jubilee kwa kushindwa kuimarisha kilimo kwa miaka 10 ikiwa uongozini na ukopaji kiholela kutoka nje.

Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Nairobi, Mhashamu Philip Anyolo Jumapili aliwakosoa wanasiasa wanaowania uongozi kwa kuwapuuza mamilioni ya Wakenya wanaohangaishwa kwa njaa.

Licha ya hali kuwa ngumu, wanasiasa wameendelea kumwaga mabilioni kwenye kampeni, wakizurura kote nchini na kutoa ahadi hewa.

Ijumaa iliyopita, wanasiasa wa Azimio la Umoja One Kenya wakiongozwa na Odinga, mgombea mwenza wake Martha Karua na Waziri wa Usalama Fred Matiang’i walikuwa na helikopta saba walipozuru Kaunti ya Nyamira.

Juni 13, 2022, viongozi hao wa Azimio walizuru Kaunti ya Kisii wakiwa na helikopta 11.

Wanasiasa wa muungano wa Kenya Kwanza nao wanapohudhuria mkutano mmoja wa kisiasa, wakiongozwa na mgombea wao Naibu wa Rais William Ruto hutumia helikopta zisizopungua tano.

Helikopta zinawezesha wanasiasa kuhutubia mikutano mingi ya kampeni au kufanya kampeni katika kaunti zaidi ya moja kwa siku.

Kwa mfano, Karua juzi Jumatatu aliandaa kampeni katika Kaunti ya Narok na baadaye katika eneo la Njoro, Kaunti ya Nakuru.

Helikopta na mabango

Inagharimu Sh170,000 (Sh3,359,661 za Tanzania) kukodisha helikopta kwa saa. Hivyo kukodisha helikopta kwa siku inagharimu kuanzia Sh1 milioni (TSh 19,762,712) kwa kuzingatia idadi ya viti. Mwaka jana pekee, wanasiasa waliagiza helikopta 41 kutoka ng’ambo wakijiandaa kwa ajili ya kampeni.

Kulingana na Mamlaka ya Safari za Ndege nchini Kenya (KCAA), helikopta mpya 325, nyingi zikiwa za wanasiasa, zilinunuliwa kati ya mwaka 2020 na 2021.

Helikopta hununuliwa kwa zaidi ya Sh202 milioni (TSh 3.99 bilioni) ughaibuni, lakini gharama huongezeka hadi zaidi ya Sh350 nchini Kenya, sawa na Sh6.92 bilioni za Tanzania.

Mbali na helikopta, wanasiasa wanatumia mamilioni ya shilingi katika kuweka mabango mijini na barabarani na kuandaa mikutano ya kampeni.

Bango moja jijini Nairobi hugharimu kati ya Sh150,000 na Sh200,000 (kati ya Sh 2.96 milioni hadi Sh3.95 milioni za Tanzania) kwa mwezi kwa kutegemea eneo na ukubwa wake.

Wagombea ugavana wameweka mabango katika kila kona katika kaunti zote na wagombea urais wameweka mamia ya mabango kote nchini katika juhudi za kujipigia debe.

Baadhi ya wanasiasa wameripotiwa kuishi katika hoteli za kifahari kukwepa wapigakura ambao wamekita kambi katika makazi yao wakitaka kupewa hela za chakula, ada na mahitaji mengineyo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *