Kwa mara nyingine, makumi ya maelfu ya wakazi wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina na kupachikwa jina la Israel wameandamana dhidi ya serikali yenye misimamo ya kuchupa mipaka ya Benjamin Netanyahu.
Maandamano ya jana Jumamosi yanahesabiwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kufanyika mjini Tel Aviv, tangu baada ya Netanyahu kurejea madarakani mwezi uliopita kuongoza baraza la mawaziri lenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia.
Duru za habari zinaarifu kuwa, waandamanaji zaidi ya 100,000 walishiriki kwenye maandamano hayo ya jana ya kulalamikia maamuzi yaliyochukuliwa na serikali ya Netanyahu ya kubana mfumo wa mahakama wa utawala huo.
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa utawala huo haramu, Yair Lapid ni miongoni mwa watu waliojitokeza kushiriki maandamano hayo ya jana Jumamosi mjini Tel Aviv.
Yariv Levin, Waziri wa Sheria katika baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu hivi karibuni aliwasilisha mpango huo kwa ajili ya kufanyia mabadiliko mfumo wa mahakama wa utawala wa Kizayuni; ambapo lengo ni kubana shughuli za mamlaka ya mfumo wa mahakama wa utawala huo.
Weledi wa mambo wanasema mpango huo unakusudia kuvuruga kanuni ya mgawanyo wa madaraka na kuliongezea uzito bunge na baraza la mawaziri mkabala wa muundo wa mahakama.
Maandamano ya jana yanaiongezea mashinikizo serikali ya Netanyahu, kwani yamejiri siku chache baada ya Mahakama ya Juu ya Israel kumuagiza Waziri Mkuu huyo kumfuta kazi Aryeh Deri, Waziri wa Mambo ya Ndani anayeongoza chama cha Shas, kwa kupatikana na hatia katika kesi ya uhujumu uchumi.