Boti yenye wakimbizi Waislamu 185 wa Rohingya imewasili katika jimbo la Aceh, nchini Indonesia.
Mamia ya wakimbizi waliwasili mwaka uliopita kutokana na hali mbaya katika kambi za wakimbizi nchini Bangladesh. Zaidi ya nusu ya wakimbizi hao waliowasili jana mchana nchini Indonesia, ni wanawake na watoto. Wengi wao wameonekana wakiwa wamelala kwenye mchanga kutokana na uchovu na udhaifu. Mamia ya wakimbizi wa Rohingya wamekuwa wakiwasili Aceh katika miezi ya hivi karibuni.
Wakimbizi 174 waliwasili sehemu hiyo mnamo mwezi Desemba mwaka uliopita. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limeatangaza kwamba mwaka 2022 huenda ulikuwa hatari sana kwa wakimbizi wa Rohingya ambao wamepitia mateso mabaya sana nchini Myanmar, yenye idadi kubwa ya mabudha.
Kwa zaidi ya muongo mmoja sasa Waislamu wa jamii ya Rohingya wanateseka kutokana na ukatili mkubwa wanaofayiwa nchini kwao Myanmar.
Itakumbukwa kuwa, Agosti 2017, zaidi ya Waislamu laki saba wa jamii ya Rohingya walilazimika kuhama makazi yao nchini Myanmar na kukimbilia kwenye kambi za wakimbizi nchini Bangladesh ili kutafuta hifadhi na kunusuru maisha yao, baada ya jeshi la Myanmar, likishirikiana na Mabudha wenye chuki za kidini, kuanzisha operesheni ya kuwaondoa kwa nguvu Waislamu hao kwa kisingizio cha mashambulizi yaliyofanywa na kundi moja la waasi.
Vikosi vya jeshi la Myanmar vimehusika na jinai mbalimbali dhidi ya Waislamu Warohingya zikiwemo za ubakaji wa halaiki, mauaji na kuchoma moto maelfu ya nyumba zao.