Mafuriko yaliyoikumba Burundi kwa takribani wiki nzima katika sehemu moja magharibi mwa nchi hiyo yamepelekea maelfu ya watu kubakia bila makazi.
Ripoti zinaeleza kuwa, katika kipindi cha wiki mafuriko yamesababisha maelfu ya familia kupoteza makazi katika eneo la magharibi mwa Burundi ambako kuna mto unatenganisha nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Afisa mmoja wa serikali ameziambia duru za habari kwamba, zaidi ya familia elfu 4 zinazoishi katika kijiji cha Gatumba zimeachwa bila makazi huku wengine wakisema wanalala nje huku wakipigwa na baridi kali nyakati za usiku.
Eneo hilo hukumbwa na hasara sawa na hiyo katika kila msimu wa mvua pale Mto Rusizi unapofurika na kuvunja kingo zake. Mto Rusizi ndio unaotenganisha Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mashirika ya misaada ya kibinadamu hapo awali yalitoa indhari kuhusu ongezeko kubwa la viwango vya maji.
Makaazi mengi ya kata tisa za kijiji cha Gatumba tarafa ya Mutimbuzi (mkoa wa Bujumbura magharibi mwa Burundi) yalivamiwa na maji ya mto Rusizi (unaotenganisha Burundi na DRC) siku chache zilizopita.
” Tunalazimika kuacha makaazi yetu na kwenda kuishi karibu na barabara. Hatuna uwezo hata wa kwenda katika mashamba yetu. Yalivamiwa na maji. Nyumba zetu zilibomoka”, alibaini Arthemon Nishimwe, mmoja wa waathirika wa mafuriko hayyo.
Anicet Nibaruta Mkuu wa Kitengo cha Kushughulikia Majanga anasema kuwa, Serikali inahitaji dola milioni 20 za Kimarekani kwa ajili ya kujenga ukuta kwenye mwambao ili kuzuia mto Rusizi kuvuka na kusababisha madhara kila mwaka unapowadia msimu wa mvua.