Somalia imetangaza habari ya kuuawa kwa magaidi 61 wa genge la al-Shabaab kusini mwa nchi, huku vikosi vya usalama vya nchi hiyo ya Pembe ya Afya vikishadidisha operesheni zao dhidi ya wanamgambo hao.
Wizara ya Habari ya Somalia imesema kuwa, magaidi hao wameuawa na Idara ya Taifa ya Intelijensia na Usalama (NISA) katika operesheni mpya iliyofanyika katika mkoa wa Shabelle ya Kati, kusini mwa nchi.
Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa, operesheni hiyo kabambe imewalenga wanamgambo wapatao 150 waliokuwa wanakula njama ya kuwashambulia askari wa serikali katika mji wa Hawadlay mkoani Shabelle ya Kati.
Abdirahman Yusuf al-Adalla, Naibu Waziri wa Habari amewaambia waandishi wa habari mjini Mogadishu kuwa, magaidi hao wa ‘Kikhawarij’ wamepata pigo kubwa katika operesheni hiyo, na njama zao za kuwashambulia maafisa usalama viungani mwa mji wa Hawadlay zimesambaratishwa.
Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Somalia Jumamosi iliyopita ilitangaza kwamba, genge hilo la kigaidi limeomba kufanya mazungumzo nayo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa magaidi hao kuomba kukutana na kuzungumza na serikali ya Mogadishu.
Aidha Jumatano iliyopita, genge hilo la ukufurishaji lilishambulia mji wa Mahas katika mkoa wa Hiran, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 35, siku moja baada ya kufanya mashambulizi makali dhidi ya vikosi vya serikali katika kijiji cha Hilowle Gaab kusini mwa mkoa wa Shabelle ya Kati.