Magaidi wa al Shabab waua watu sita katika uvamizi wa kijiji kimoja nchini Somalia

Genge la kigaidi na ukufurishaji la al Shabab limeua takriban watu sita katika shambulizi dhidi ya kijiji kimoja cha katikati mwa Somalia ambacho walifurushwa wiki iliyopita.

Hayo yamethibitishwa na wapiganaji wa kieneo wanaoiunga mkono serikali ya Somalia na kuongeza kuwa, shambulio hilo limetokea katika kijiji cha Hilowle Gaab katika Jimbo la Hirshabelle, ambacho jeshi la Somalia lilikikomboa kutoka kwa magaidi al Shabab wiki iliyopita.

Hussein Aden, msemaji wa wapiganaji wa eneo hilo amesema, magaidi wa al Shabab walishambulia kijiji hicho jana Ijumaa wakati wa sala ya alfajiri kwa kutumia magari na mabomu.

“Baada ya miripuko hiyo kumetokea mapigano ya risasi na magaidi wa al Shabab wamefurushwa,” amesema.

“Tuliamshwa na miripuko mitatu yenye sauti kubwa ya kutia uziwi, nje ya kijiji chetu, kisha yakafuatia majibizano makubwa ya risasi,” amesema Mohamed Hussein, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho cha Hilowle Gaab

Genge la al Shabab lilidai hiyo jana katika taarifa yake kwamba limekiteka tena kijiji pamoja na magari ya kijeshi na silaha, lakini wakaazi wa kijiji hicho wamepinga vikali madai hayo ya uongo ya magaidi wa al Shabab.

Genge la al Shabab lililojitangaza rasmi kuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al Qaida limekuwa likifanya jinai na mauaji makubwa ndani ya nje ya Somalia tangu mwaka 2007.

Licha ya genge la ukufurishaji la al Shabab kutimuliwa katika miji mikubwa na vituo muhimu vya Somalia takriban miaka 10 iliyopita, lakini bado vitendo vya kikatili vya magaidi hao vinashuhudiwa kwenye vijiji vingi vya katikati na kusini mwa Somalia.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *