Magazeti na vyombo vingine vya habari vya nchi za Afrika Mashariki vimeakisi kwa mapana safari ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye leo Jumanne anatazamiwa kuondoka nchini kuelekea barani Afrika kwa ziara ya siku tatu ya kuzitembelea nchi za Kenya, Uganda na Zimbabwe.
Sehemu ya juu ya ukurasa wa mbele wa gazeti la Daily Nation chapisho la leo Jumanne, kuna picha ya Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, iliyoambatana na anuani isemayo: Rais wa Iran aanza safari ya siku tatu nchini Kenya.
Maelezo kamili kuhusu safari hiyo ya Rais wa Iran katika nchi tatu hizo za Kiafrika na hasa uhusiano wa kisiasa na kibiashara baina ya Jamhuri ya Kiislamu na Kenya yapo katika ukurasa wa tisa wa gazeti hilo.
Gazeti la Daily Monitor la Uganda limeandika habari kuhusu safari hiyo ya Sayyid Raisi chini ya kichwa kisemacho: Rais wa Iran kuzitembelea nchi za Kenya, Uganda na Zimbabwe.
Limenukuu shirika la habari la IRNA lililoripoti kuwa, Rais Raisi anaandamana na ujumbe wa ngazi za juu wa maafisa wa serikali ya Iran, akiwemo Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu, pamoja na wawekezaji na wafanyabiashara waandamizi wa Iran.
Alireza Peyman Pak, Katibu wa Baraza Kuu la Usimamizi la Chama cha Wafanyabiashara wa Iran, anasema kuhusu uhusiano wa Iran na Afrika kwamba: Uanzishwaji wa usafirishaji wa uhakika wa meli, ujenzi wa miundombinu na kusainiwa makubaliano ya kupunguza ushuru wa biashara, vinaweza kuwa na taathira kubwa katika kuzidisha biashara kati ya Iran na bara la Afrika.”
Mbali na umuhimu wa kiuchumi wa uhusiano wa Iran na bara la Afrika, kustawishwa uhusiano na nchi za bara hilo katika masuala ya siasa na utamaduni pia kuna umuhimu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo imewekewa vikwazo na mashinikizo ya kisiasa ya nchi za Magharibi.