Mageuzi ya Bin Salman huko Saudi Arabia ni ya uongo na bandia

“Rima bint Bandar Al Saud”, balozi wa Saudi Arabia nchini Marekani, alitangaza karibuni katika mahojiano na CNN, kwamba mageuzi ya Saudi Arabia ni ya kweli na kwamba ufalme huo umechukua hatua katika miaka mitano iliyopita ambayo ilikuwa haijafanyika katika miaka 80 iliyopita

Katika kujibu matamshi hayo, Shirika la Haki za Kibinadamu la Ulaya-Saudia limetaja mageuzi ya Mwana Mfalme wa Saudia Mohammad Bin Salman (MBS) kuwa ya uwongo na bandia.

Mohammed bin Salman aliteuliwa kuwa Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia mnamo Juni 2017. Tokea wakati huo Bin Salman ameondoa vikwazo katika nyanja za kijamii. Kwa mfano, amewapa wanawake haki ya kuendesha magari, kutoa vibali vya kufanyika matamasha, kuruhusu wanawake kuhudhuria mechi za soka katika viwanja n.k.

Bin Salman anaziita hatua hizo, ambazo baadhi ni haki za kimsingi za kila raia, wakiwemo wanawake, kuwa ni mageuzi katika hali ambayo hajachukua hatua yoyote ya kuwapa wanawake wa Saudia haki zao za kisiasa.

Suala muhimu zaidi ni kwamba kimsingi wachambuzi wa masuala ya uhusiano wa kimataifa na sheria za kimataifa sio tu kwamba hawamchukulii Muhammad bin Salman kuwa kiongozi wa mageuzi, bali pia wanamwona kuwa ni kiongozi dikteta, wa kimabavu na mmoja wa wavunjaji wakuu wa haki za binadamu duniani.

Rais wa Marekani Joe Biden alitangaza rasmi katika kipindi cha kampeni za uchaguzi wa rais kwamba ataigeuza Saudi Arabia kuwa nchi iliyotengwa. Sababu kuu ya maoni hayo ya Biden ilikuwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu wa serikali ya Saudia. Kwa hiyo, yale madai ya mageuzi ya Bin Salman hayakukubaliwa hata na muungaji mkono mkuu wa Saudi Arabia katika uga wa kimataifa.

Mbali na kuondoa baadhi ya vizuizi vya kijamii, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia ameongeza hali ya ukandamizaji wa kisiasa ambapo wapinzani hawapati mwanya wa kupaza sauti zao.

Kuhusiana na hilo, Shirika la Haki za Kibinadamu la Ulaya-Saudia, ambalo linashughulikia kesi za ukiukaji wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia, limetangaza katika taarifa yake kwamba, kuongezeka kwa visa vya ukiukaji wa haki za binadamu katika miaka ya hivi karibuni, kuanzia kukamatwa kiholela hadi hukumu ndefu dhidi ya wanaharakati wa haki za binadamu, unyongaji usio wa haki , uhamaji wa kulazimishwa wa wanaharakati na ukandamizaji wa taasisi za kiraia zote zinaonyesha kuwa mabadiliko yanayodaiwa hayawezi kuchukuliwa kuwa mazuri wala kuitwa kuwa ni mageuzi ya msingi.

Shirika hilo linasisitiza kuwa, mabadiliko ambayo ufalme wa ukoo wa Aal Saud unajivunia kuwa umeyafanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ni pamoja na kuongezeka maradufu idadi ya hukumu za kifo, ambazo ni sawa na hukumu elfu moja zikiwemo hukumu za kifo dhidi ya watoto.

Miongoni mwa watu waliokabiliwa na ghadhabu za utawala wa Saudia, wamo watu wa matabaka mbali mbali ya kijamii wakiwemo wanawafalme wa Saudia, wanaharakati wa kiraia na kidini, raia wa kawaida wanaopinga hali mbaya ya maisha na hata baadhi ya mamufti.

Miongoni mwa watu hao, wapo pia watu waliotetea haki za wanawake nchini Saudi Arabia, lakini wako jela, wanateswa na kunyimwa haki yao ya kuishi. Kwa hivyo, alichokifanya Muhammad bin Salman huko Saudi Arabia katika miaka ya hivi karibuni hakikuwa mageuzi na kuzingatia maadili ya haki za binadamu, bali ni vitendo vinavyolenga kupata umaarufu na kukubalika kwa kizazi kipya cha Saudi Arabia. Ni wazi kuwa ukandamizaji wa kimfumo umeongezeka zaidi katika nchi hiyo ya kifalme chini ya utawala wa Bin Salman.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *