Mahakama ya Juu Kenya yatupilia mbali kesi ya Odinga, yabariki ushindi wa Ruto

Mahakama ya Juu nchini Kenya imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa na mgombea wa urais wa Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Mgombea kiti cha urais kwa tiketi ya Muungano wa Azimo One Kenya Raila Odinga aliitaka Mahakama ya Juu ya Kenya kutupilia mbali ushindi wa William Ruto wa Muuungano wa Kenya Kwanza au kumtangaza yeye kama mshindi katika uchaguzi wa rais wa tarehe 9 mwezi Agosti huku mojawapo ya kesi zilizowasilishwa mahakamani humo ikidai kwamba hakuna yeyote kati ya wawili hao aliyepata asilimia hamsini na kura moja.

Katika uamuzi wa jopo la majaji saba wa mahakama hiyo uliosomwa na Jaji Mkuu (CJ), Martha Koome hii leo, kwa kauli moja wamesema malalamishi ya Raila hayakuishawishi korti kubatilisha ushindi wa Dkt Ruto.

Raila pamoja na walalamishi wengine waliibua matakwa tisa wakihoji uchaguzi ulikumbwa na udanganyifu na kasoro nyingi.

“Kwenye uamuzi wa pamoja wa korti, Rais Mteule William Ruto alichaguliwa kihalali,” ametangaza Koome leo Jumatatu katika maamuzi yaliyosomwa kwa zaidi ya saa moja.

Mahakama ya Upeo ilipuuzilia mbali matakwa yote tisa yaliyoibuliwa na mlalamishi, ikisema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilizingatia sheria na vigezo vya uchaguzi.

Agosti 15, mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alimtangaza Dkt Ruto aliyegombea kupitia muungano wa Kenya Kwanza kama Rais Mteule.

Ruto ambaye kati ya 2013 na 2022 alihudumu kama naibu wa rais, alizoa kura 7, 176, 141 kiwango kinachowakilisha asilimia 50.49 ya idadi jumla ya kura zilizopigwa. Raila alipata kura 6, 942, 930, sawa na asilimia 48.85.

Mahakama ya Kilele ya kenya imesema Ruto aliafiki kigezo cha Katiba, cha kupata asimilia 50 ya kura halali zilizopigwa na kura moja au zaidi. Odinga ambaye ni mwanasiasa mkongwe mwenye umri wa miaka 77 alisema makamishna wa tume hiyo hawakukubaliana kuhusu hesabu ya mwisho ya matokeo hayo yaliyompatia ushindi mshindani wake mkuu William Ruto.

Mahakama ya Upeo ya Kenya imesema kila upande ulioshiriki, utagharimia malipo ya kesi. Aidha, maelezo ya kina kuhusu maamuzi hayo yatatolewa baada ya siku 21.

Dakta Ruto sasa anatazamiwa kuapishwa Septemba 13.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *