Mahakama ya Juu ya India yamtaka msemaji wa zamani wa chama tawala kuomba radhi kwa kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw)

Mahakama ya Juu ya India imemtaka msemaji wa zamani wa chama tawala nchini India cha Bharatiya Janata kinachoongozwa na Waziri Mkuu, Narendra Modi, Nupur Sharma, kujitokeza kwenye televisheni na kuomba radhi kwa taifa zima la India, baada ya matamshi yake ya kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) ambayo yameisababisha maandamano makubwa na kuchochea hali ya mvutano nchini humo.

Matamshi hayo pia yamezusha mgogoro katika uhusiano wa kidiplomasia wa India na baadhi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu.

Mahakama ya Juu ya India imekosoa vikali matamshi ya Nupur Sharma ikimtaja kuwa ni mpayukaji. Imesema msemaji huyo wa zamani wa chama tawala anabeba peke yake dhima ya machafuko na mivutano inayojiri nchini India.

Taarifa ya mahakama hiyo imesema: “Sharma na ulimi wake ameiteketeza nchi, anawajibika kwa yale yanayojiri nchini na anapaswa kuomba radhi kutokana na matamshi yake.”

Hasira ilitanda India na Ulimwengu wa Kiislamu mwezi uliopita baada ya Sharma kutoa matamshi ya matusi na kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) wakati wa mjadala wa televisheni, ambapo karibu nchi 20 ziliwaita mabalozi wa India kwa ajili ya kupata maelezo.

Maandamano makubwa ya Waislamu yalishuhudiwa katika nchi kadhaa ikiwemo Pakistan, India, Iran, Indonesia, na Banghladesh ambako Waislamu walitoa wito wa kususiwa bidhaa za India kutokana na matamshi hayo machafu ya msemaji wa chama tawala.

Nchini India kwenyewe, waandamanaji wasiopungua wawili waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi, huku nyumba kadhaa za Waislamu zikibomolewa kwa mabuldoza, katika kile wakosoaji walichokiita “adhabu ya halaiki” inayotolewa mamlaka kwa watu walioshiriki maandamano.

Mwezi uliopita wa Juni Taasisi ya Haki za Binadamu ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ililaani vitendo vya kibaguzi dhidi ya Waislamu nchini India.

Taasisi hiyo ilitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuiwajibisha India kwa ukiukaji wa haki za binadamu za walio wachache na kukomesha uhasama wake.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *