Mahakama ya Mali yamhukumu kifo mtu mmoja kwa vifo vya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa

Mahakama nchini Mali imemhukumu kifo mwanaume mmoja kwa kuhusika katika shambulio mwaka 2019 lililouwa wanajeshi watatu wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa. Hayo yameelezwa na kikosi cha kulinda amani cha UN nchini Mali (MINUSMA)

Mali ambayo inaongozwa na serikali ya kijeshi kwa muongo sasa imekuwa ikipambana na hali ya mchafukoge inayosababishwa na makundi yanayobeba silaha katika maeneo mbalimbali nchini humo. Ukosefu wa usalama ulioiathiri Mali umeenea pia hadi katika eneo la Sahel licha ya jitihada kubwa za kimataifa za kukomesha hali hiyo.

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Mali kinajumuisha askari jeshi wa mataifa kadhaa (MINUSMA) kimekuwa kikidumisha usalama nchini humo tangu mwaka 2013. Hata hivyo uwepo wa kikosi hicho umeshindwa kuzuia hujuma na mashambulizi ya makundi yenye silaha yenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida na kundi la Daesh (ISIS) dhidi ya vijiji, miji, kambi za jeshi na vituo vya polisi nchini.

Mwanaume huyo amehukumiwa kifo katika kesi inayohusiana na shambulio dhidi ya walinda amani watano waliokuwa wakisafiri katika eneo la Siby kusini mwa Mali, karibu kilomita 50 kutoka mji mkuu Bamako mnamo Februari 22, 2019. Wanajeshi watatu kutoka Guinea waliuawa. Inafaa kuashiria hapa kuwa, Guinea ni kati ya nchi zilizotuma idadi kubwa ya walinda amani katika kikosi cha MINUSMA huko Mali.

Mahakama ya jinai ya Bamako imemtia hatiani mwanamume huyo kwa kushiriki vitendo vya uhalifu, mauaji, wizi na kumiliki silaha kinyume cha sheria katika shambulio dhidi ya walinda amani huko Siby. Majaji wa mahakama ya Bamako wamemhukumu kifo mhalifu huyo; ambayo haijatekelezwa nchini Mali tangu kusitishwa kwake mwaka 1980.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *