Mahakama nchini Burundi imethibitisha kifungo cha maisha jela dhidi ya jenerali Alain Guillaume Bunyoni waziirii mkuu wa zamani wa nchi hiyo.
Alipatikana na hatia mwezi Disemba mwaka jana kwa makosa mengi ya jinai ikiwa ni pamoja na kujaribu kupindua serikali, kumiliki utajiri kinyume cha sheria, kuhujumu uchumi na vitisho kwa maisha ya rais na taasisi za serikali.
Pamoja na kifungo cha maisha jela, mahakama imemuamuru kulipa faini ya zaidi ya dola 7,893,326 na kuzuiwa kwa mali yoyote ambayo hakuieleza mahakama mnamo Juni 2021.
Jenerali huyo wa zamani wa jeshi aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa Burundi mnamo Julai 2020 na kufukuzwa kazi mnamo Septemba 2022.
Kuondolewa kwake kulikuja siku chache baada ya Rais Evariste Ndayishimiye kuonya juu ya kile alichokiita njama ya “mapinduzi” dhidi yake.
Katika hukumu yake hiyo, mahakama iliagiza pia mamlaka husika kutaifisha mali za waziri mkuu huyo wa zamani ambazo ni nyumba na majengo manne pamoja na eneo la ardhi na magari 14.
Kwa mujibu wa duru za mahakama, washtakiwa wengine watano waliopandishwa kizimbani wakiwemo washitakiwa wenza wakuu wawili, kanali wa polisi na afisa mwandamizi wa intelijensia, wamehukumiwa vifungo vya kuanzia miaka mitatu hadi 15 jela. Duru hiyo imeongeza kuwa, mshtakiwa wa saba ambaye ni dereva ameachiwa huru. Akiwa mshirika wa karibu wa rais wa zamani Pierre Nkurunziza, Bunyoni alikuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa katika chama tawala cha CNDD-FDD.