Mahakama yazuia polisi wa Kenya kutumwa nchini Haiti

Mahakama ya juu nchini Kenya imetangazwa kuwa, mpango wa serikali katika taifa hilo la Afrika Mashariki wa kuwatuma polisi nchini Haiti kuongoza kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa ni kinyume na katiba.

Kenya ilikuwa imekubali kuwatuma polisi elfu moja nchini Haiti kusaidia kurejesha usalama pamoja na kupambana na makundi ya watu wenye silaha.

Novemba mwaka jana (2023) Bunge la Kenya liliidhinisha kutumwa kwa maafisa wa polisi elfu moja katika nchi ya Haiti iliyotumbukia katika machafuko na ghasia za magenge yenye silaha.

Uamuzi huu wa mahakama unakuja wakati huu ambapo serikali ya Haiti inatoa wito kwa jamii ya kimataifa kutuma kikosi chake kuwasaidia maofisa wake ambao wameonekana kuzidiwa na magenge.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Haiti Jean Victor Geneus, ameomba kutumwa kwa kikosi cha kimataifa katika nchi hiyo inayokabiliwa na mzozo na kuliambia Baraza la Usalama la UN kwamba ghasia za magenge nchini humo ni za kinyama

Wakati huo huo mahakama ya rufaa nchini Kenya, imeamua kuwa mpango wa utozwaji kodi unaotekelezwa na serikali ya Rais William Ruto ili kujenga makaazi yenye bei nafuu, ni kinyume cha sheria.

Serikali ilikuwa imeiomba mahakama kuiruhusu kuendelea kutoza ushuru huo kutoka kwa mapato ya kila mwezi kutoka kwa raia walioajiriwa wakati ikisubiri kusikilizwa kwa rufaa ya kupinga mpango huo wa utawala wa rais Ruto.

Mwezi Juni mwaka uliopita (2023), Rais William Ruto alitia saini sheria ya fedha ya mwaka wa 2023, ambayo inapingwa na kulalamikiwa na baadhi ya raia na mrengo wa upinzani unaoongozwa na Raila Odinga.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *