Maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walitumia uwezo na nguvu zao zote katika machafuko ya hivi karibu kujaribu kutoa pigo kwa Iran ya Kiislamu, lakini kama ilivyojiri kwa miaka ya huko nyuma, njama zao za mara hii pia zimesambaratika na kwa mara nyingine umoja na mshikamano wa wananchi pamoja na nguvu na uimara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umefelisha njama hizo.
Pamoja na kwamba tangu mwanzoni kabisa mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kisilamu na kuvurugika milingano ya ubeberu wa kimataifa hadi hivi sasa, Iran imekumbwa na mawimbi makubwa makubwa ya chuki na uhasama wa maadui na vibaraka wao vikiwemo vijigenge vyao vya kigaidi, lakini katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, maadui wameendesha vita vikubwa mseto kwa kutumia nguvu zao zote za kisiasa, kiuchumi, kimawasiliano na mabanda yao ya propaganda dhidi ya Iran. Ushahidi wa wazi kabisa unaonesha kuwa, katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, Shirika la Kijasusi la Marekani CIA kwa kushirikiana na mashrika mengine ya kijasusi ya waitifaki wake yametumia magenge na tawala zenye fikra mgando za eneo hili kuchochea na kufanya fujo na mauaji ndani ya Iran ili kuongeza mashinikizo kwa taifa hili, lakini njama zote hizo zimeshindwa.
Mashirika ya kijasusi ya Magharibi na ya Kizayuni yamefikia hata kutoa mafunzo maalumu ya vita mseto kwa vitimbakwiri na vibaraka wao ili kuvuruga utulivu na amani nchini Iran. Njia nyingine kuu iliyotumiwa na mashirika ya kijasusi ya maadui wa Jamhuri ya Kiislamu kwa ajili ya kuchochea vujo na machafuko nchini Iran mara hii, ni kuchochea hisia za kikaumu na za matabaka mbalimbali ya wananchi kama walimu, wafanyakazi na wanafunzi. Mashirika hayo ya kijasusi yalianzisha makundi bandia na machafu kwa ajili ya kuyatumia vibaya kuzusha ghasia. Wakati huo huo nchi za Magharibi tangu mwanzoni kabisa mwa machafuko hayo ya hivi karibuni ya nchini Iran, zilitangaza uungaji mkono wao kamili kwa wafanya vurugu ili kushadidisha mashinikizo yao ya kiuchumi na kisiasa dhidi ya Iran kwa visingizio chapwa kama vya haki za binadamu. Lengo lao hasa ni kuidhoofisha Jamhuri ya Kiislamu kimataifa na wakati huo huo kuchochea malalamiko ndani ya nchi. Ni jambo lisilo na shaka kwamba, pamoja na adui – yaani nchi za Magharibi, utawala wa Kizayuni wa Israel na vibaraka wao wa eneo hili yaani baadhi ya tawala zenye fikra mgando za nchi za Kiarabu – kuja kwa nguvu zote hizo za mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na kipropaganda, lakini kuwa macho wananchi wa Iran na umakini wa hali ya juu wa Iran ya Kiislamu wa kupambana na masuala ya kijasusi na kiusalama, kwa mara nyingine tena vimesambaratisha na kufelisha njama hizo kubwa na za kila upande za adui. Pamoja na hayo lakini, uzoefu wa kihistoria unaonesha kuwa, adui muda wote hutumia fursa yoyote ile hata ndogo kupindukia, kujaribu kutoa pigo kwa Iran ya Kiislamu na kwa malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu. Hivi sasa njama hizo za adui zinalenga zaidi kwenye kuchochea wananchi ili wasimame dhidi ya Jamhuri ya Kisilamu ya Iran. Jana Alkhamisi, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aligusia kushindwa tena adui katika matukio ya hivi karibuni ya nchini Iran na kusisitiza kwa kusema: “Kwa muda wa miaka 40 sasa wanatumia kila njia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini kwa vile mahesabu yao ni mabovu, hadi sasa wameshindwa na katika siku za usoni pia watashindwa.”
Pamoja na hayo, Kiongozi Muadhamu amesisitiza pia kwamba, ijapokuwa mahesabu ya adui ni mabovu, lakini hatupaswi kughafilika naye. Amesema: “Sisi pia tunapaswa kuwa makini. Isiwe ni kukumbwa na mghafala, ghururi na majivuno na kusema, mambo yameisha. Lazima tubaki imara kwenye medani ya mapambano na tutambue kuwa, sababu ya kulindwa taifa hili, ni matumaini na mshikamano wake wa kitaifa.”