Mahmoud Abbas: Marekani na Uingereza zinapaswa kuomba radhi kwa taifa la Palestina

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameitaka jamii ya kimataifa isishirikiane na serikali haramu za utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema: Marekani na Uingereza zinapaswa kuomba radhi kwa watu wa Palestina.

Mahmoud Abbas amesema katika kikao cha pamoja cha nchi za Kiarabu na China mjini Riyadh kwamba, Marekani na Uingereza zinapaswa kuwaomba radhi wananchi wa Palestina na kuwalipa fidia kutokana na kutia saini Azimio ovu la Balfour.

Abbas ameongeza kuwa, utendaji wa mfumo wa kimataifa unaofumbia macho jinai za Israel dhidi ya wananchi na maeneo matakatifu ya Palestina na kutazama tu kwa macho uvamizi wa utawala ghasibu katika ardhi ya Palestina kwa miaka kipindi cha 74 kwa hakika ni jambo linalozua maswali mengi.

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema: Tunaiomba jamii ya kimataifa isishirikiane na serikali yoyote ya Israel ambayo haiheshimu maadili na sheria za kimataifa.

Mahmoud Abbas amesema: “Tutaendelea kushikamana na haki ya uanachama wa palestina katika Umoja wa Mataifa na tunataka uungwaji mkono wa kimataifa kwa watu wa Palestina.”

Kiongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameongeza kuwa, Watu wa Palestina wanasimama pamoja na Beijing katika kuunga mkono sera ya China Moja na wanapongeza misimamo thabiti ya Rais wa China ya kuliunga mkono taifa la Palestina.

Azimio la Balfour ni mojawapo ya hatua za aibu zaidi katika historia ya nchi za Magharibi na linajulikana kama msingi wa kihistoria wa kuundwa kwa taifa bandia la Wayahudi katika ardhi za Palestina.

Awali, ilifikiriwa kuwa Azimio la Balfour lilikuwa kitendo cha Uingereza tu, lakini hati rasmi zilizofichuliwa baadaye zilithibitisha kuwa Azimio hilo liliwasilishwa kwa Marekani na kwamba nchi hiyo ililikubali. Pia, mnamo 1918, Ufaransa na Italia zilitangaza kuunga mkono Azimio la Balfour.

Azimio hilo ni barua iliyoandikwa na Arthur James Balfour, waziri wa mambo ya nje wa wakati huo wa Uingereza, tarehe 2 Novemba 1917, kwa Walter Rothschild, mwanasiasa mwenye asili ya Kiyahudi na mmoja wa wafuasi mashuhuri wa Uzayuni, ambamo Wayahudi waliahidiwa kuunda “taifa” katika ardhi ya Palestina. Hatua hii ilichukuliwa wakati wakazi wa Kiyahudi huko Palestina walikuwa asilimia tano tu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *