Majaji wa Umoja wa Mataifa wameamuru kesi ya uhalifu wa kivita inayomkabili mshukiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, Felicien Kabuga mwenye umri wa miaka 90 isitishwe kwa muda usiojulikana kwa sababu ana matatizo ya akili.
Uamuzi huo huenda una maana kuwa kesi ya Kabuga, iliyoanza mwaka jana huko The Hague, haitakamilika.
Mwezi Juni, majaji katika Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya Umoja wa Mataifa waliamua kuwa Felicien Kabuga hafai kufikishwa mahakamani kutokana na ugonjwa wa akili lakini walipendekeza taratibu mbadala zifanyike. Kwa sasa majaji wa rufaa wamekataa pendekezo hili.
Kwa mujibu wa majaji hao, Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya Umoja wa Mataifa ilifanya “kosa la sheria” mwezi Juni kwa kuamua kwamba Félicien Kabuga anapaswa kushitakiwa kupitia utaratibu mbadala uliorahisishwa licha ya hali yake ya afya. Na sasa mahakama ya mwanzo imeamrishwa kuhakikisha Kabuga anaachiliwa huru.
Mfanyabiashara huyo aliyekuwa pia akimiliki kituo cha redio kilichotuhumiwa kuhamasisha mauji ya kimbari dhidi ya Watutsi hapo mwaka 1994 nchini Rwanda, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 80, ni mmoja wa washukiwa wakuu wa mwisho wanaosakwa na mahakama hiyo inayochunguza uhalifu uliofanywa wakati wa mauaji hayo ya kimbari.
Anatuhumiwa kueneza chuki na mauaji kupitia kituo chake cha redio na kuwahamasisha wauaji waliowaua zaidi ya watu 800,000 katika kipindi cha siku 100 tu. Alikamatwa mjini Paris mwaka 2020, baada ya miongo miwili ya kuwa mafichoni. Bw Kabuga alikanusha mashtaka.
Hata hivyo Mahakama ya Umoja wa Mataifa imekiri kuwa, uamuzi wa kuachiwa huru Felicien Kabuga utawakatisha tamaa wahanga na manusura wa mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi.