Majambazi wateka nyara watu 63 nchini Nigeria baada ya kushambulia maficho yao

Watu wenye silaha, ambao wenyeji wanaamini ni majambazi wameteka nyara makumi ya wakazi wa Jimbo la Niger nchini Nigeria baada ya vikosi vya usalama kuokoa watu wengine 13.

Ingawa msemaji wa polisi, Wasiu Abiodun, amekataa kuthibitisha ni watu wangapi hasa waliotekwa nyara katika jamii tatu za jimbo hilo la Niger, lakini baadhi ya duru za usalama zimefichua kuwa idadi ya watu hao ni 63.

Tukio hilo limetokea katika eneo la Pandogari la kaskazini mashariki mwa jimbo hilo la Niger huko Nigeria na limetokea kilomita chache tu kutoka kambi moja ya askari wa serikali.

Watu 41 wametekwa nyara katika kijiji cha Durmin, huku 14 wakichukuliwa mateka katika kijiji cha Jarmiya na wanane katika kijiji cha Pandogari.

Msemaji wa polisi, Wasiu Abiodun, amesema maafisa usalama wameokoa takriban watu 13 katika maficho ya watu wenye silaha, wanaoaminika ni majambazi. Baada ya tukio hilo majambazi hao walilipiza kisasi kwa kuwateka nyara makumi ya watu wengine wa jimbo hilo.

Viongozi wa serikali wamesema kuwa wameongeza msako wa kuwasaka majambazi hao na timu mbalimbali zimeundwa kushughulikia jambo hilo.

Kiongozi wa mmoja wa kijiji cha Durmin, Adamu Dangana, ameiliambia shirika la habari la Anadolu kwamba majambazi hao walivamia maeneo hayo wakiwa wanaendesha pikipiki na idadi yao ilikuwa kubwa sana.

Dangana amesema majambazi hao walikuwa na silaha mbalimbali zikiwemo bunduki aina ya AK-47, na kutishia kumpiga risasi yeyote aliyekaidi amri zao. Amesema: “Nilifanikiwa kujificha katikati ya mifugo ya mbuzi ili kuepuka kutekwa nyara.”

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *