Makadirio ya zaidi ya dola bilioni 80 za mashambulio ya utawala wa Kizayuni Gaza

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa kutokana na mashambulizi ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza, ukarabati na ujenzi mpya wa ukanda huo utagharimu zaidi ya dola bilioni 80 na mchakato huo kuchukua miongo minane kukamilika.

Katika hali ambayo Ukanda wa Gaza unakabiliwa na uharibifu mkubwa na tani milioni 42 za vifuzi na uchafu ambao umekusanyika katika ukanda huo, gharama ya kujenga upya magofu na majengo yaliyoharibiwa unakadiriwa kugharimu dola bilioni 80. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, tani milioni 42 za uchafu zimerundikana katika maeneo tofauti ya Gaza kutokana na zaidi ya asilimia 70 ya nyumba na majengo kuharibiwa. Hali hii imepelekea wahandisi kueleza ujenzi wa Gaza kuwa jambo lisilowezekana.

Tathmini za kimataifa, zikiwemo za Umoja wa Mataifa, zinaonyesha kuwa gharama ya kuijenga upya Gaza itafikia zaidi ya dola bilioni 80, na kuondolewa vifuzi na uchafu uliokusanyika katika ukanda huo kuchukua miaka mingi, ambapo gharama yake inakadiriwa kufikia dola milioni 700. Umoja wa Mataifa umetabiri kuwa, itachukua miongo minane kurejesha Gaza katika hali iliyokuwepo kabla ya kuanza vita vya mauaji ya kimbari na ukatili wa kutisha unaofanywa katika ukanda huo na utawala wa kibaguzi wa Israel.

Mchakato wa kuondoa vifuzi na uchafu huko Gaza unazidi kuwa mgumu kutokana na kuwepo mabomu ambayo hayajalipuka bado, vifaa hatari na mabaki ya miili chini ya vifusi. Ripoti ya Umoja wa Mataifa inakadiria kuwa tani zisizopungua milioni 8.5 za vifusi lazima ziondolewe huko Khan Younis, wakati hali ya kaskazini mwa Gaza ni hatari sana ambapo eneo hilo linakabiliwa na uharibifu mkubwa. Zaidi ya nusu ya vifusi vya Gaza inapatikana katika eneo hili.

Utawala wa Kizayuni tangu kuanza operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa cha makundi ya muqawama ya Palestina tarehe 7 Oktoba 2023, umekuwa ukilenga mara kwa mara miundombinu ya kibinadamu huko Gaza zikiwemo shule na hospitali kwa uungaji mkono na ushirikiano kamili wa Marekani. Mashambulio ya utawala wa Kizayuni kuanzia tarehe 7 Oktoba 2023 hadi Julai 27, 2024 yamelenga maeneo yaliyopigwa marufuku kushambuliwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa za vita, zikiwemo shule 564 za Ukanda wa Gaza.

Utawala wa Kizayuni pia umefanya mashambulizi kinyume cha sheria dhidi ya hospitali na vituo vya matibabu vinavyofungamana na Umoja wa Mataifa. Mbali na idadi kubwa ya mashahidi wa Kipalestina waliouawa katika mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni ambao wengi wao ni wanawake na watoto, miundombinu ya afya na elimu pia imekuwa shabaha kuu ya Wazayuni.

Wazayuni wanalenga kwa makusudi shule za Gaza, ambayo ni makaazi ya muda ya wakimbizi wa Kipalestina waliopoteza makaazi yao kutokana na mashambulio ya jeshi la Israel.

Hali ya mambo huko Gaza ni ishara ya jinai na uharibifu mkubwa unaofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestinba kwa uungaji mkono wa Marekani, ambapo Tel Aviv na Washington zinapaswa kuwajibishwa kuhusiana na mgogoro wa kibinadamu na kiuchumi wa Gaza na vilevile kutokana na kuhusika kwao katika mauaji ya kimbari na uharibifu wa makusudi huko Gaza.

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa za vita, kushambuliwa shule, hospitali na maeneo ya makazi ya raia kunachukuliwa kuwa jinai za kivita ambapo wahusika wanapaswa kuhukumiwa na kuadhibiwa katika mahakama za kimataifa. Viongozi wa utawala wa Kizayuni ndio wahusika wakuu wa mauaji ya kimbari na uharibifu unaoendelea huko Gaza na wanapaswa kuwajibishwa kuhusiana na jinai hizo. Uharibifu mkubwa wa miundombinu ya kibinadamu pia unahesabiwa kuwa jinai ya kivita, ambapo utawala wa Kizayuni na Marekani zinalazimika kisheria kufidia na kuwalipa watu wa Palestina hasara kubwa ya kifedha iliyosababishwa na uharibifu huo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *