Makampuni ya Oman na Kuwait yajiondoa kwenye maonyesho ya Bahrain kuisusia Israel

Shirika la ndege la bei nafuu la Oman na Benki ya Kiislamu ya Kuwait zimeamua kujiondoa katika maonyesho yajayo ya Kimataifa ya Anga ya Bahrain (BIAS) baada ya kubaini wajumbe kutoka makampuni ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel watashiriki katika maonyesho hayo, ikiwa ni hatua ya kuonyesha mshikamano na uungaji mkono kwa Palestina.

SalamAir, imeeleza katika tangazo ililoweka kwenye ukurasa wake wa Twitter, kwamba inajiondoa kwenye maonyesho ya sita ya kimataifa ya Anga ya Bahrain, ambayo yamepangwa kufanyika kuanzia Novemba 9 hadi 11, na kufunga banda lake ililotengewa kwenye maonyesho hayo.

Nayo Finance House, benki ya kwanza ya Kiislamu ya Kuwait iliyoanzishwa mwaka 1977 imetangaza kuwa imechukua uamuzi sawa na huo.

Kundi la Muungano wa Ghuba ya Uajemi linalopinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya nchi za Kiarabu na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel limethibitisha kushiriki makampuni kadhaa ya utengezaji silaha ya Israel katika maonyesho ya anga ya Bahrain.

Kwa mujibu wa kundi hilo, makampuni hayo ndiyo yanayounda ndege za kivita na silaha mbalimbali za maangamizi kwa ajili ya jeshi la Israel ili kubomolea nyumba za Wapalestina na kuua makumi ya raia wakati wa hujuma ya kinyama ya kijeshi ya siku 11 kwenye Ukanda uliozingirwa wa Gaza mnamo Mei 2021.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *