Utawala wa Kizayuni umeafiki mpango wa jumla wa kuikabidhi nchi ya Saudi Arabia visiwa viwili vya Misri.
Shirika la Habari la Kimataifa la Fars limetoa ripoti kua; tovuti ya Marekani imeripoti kuwa, utawala wa Kizayuni umeafiki mpango wa jumla kuhusu hadhi ya kisheria ya visiwa viwili vya Misri katika Mlango wa Bahari wa Tiran. Hatua hii inafungua njia ya kuhalalisha uhusiano kati ya Riyadh na Tel Aviv.
Makubaliano hayo, ambayo yamejadiliwa kisiri kwa miezi kadhaa, yatakuwa mafanikio muhimu ya sera za kigeni kwa utawala wa Joe Biden katika eneo la Asia Magharibi, kulingana na Axios.
Makubaliano hayo pia yanaweza kuandaa njia kwa makubaliano tofauti ambayo yataruhusu ndege za Israel kutumia anga ya Saudi Arabia kuruka India au China.
Maafisa wa Kizayuni wamesema kuwa makubaliano hayo yanatarajiwa kutangazwa katika ziara ya Joe Biden nchini Saudi Arabia katika siku zijazo. Maafisa hawa walisema kwamba Tel Aviv ilitoa mwanga wa kijani kwa makubaliano haya kwa Marekani siku ya Alhamisi.
Masharti ya makubaliano hayo katika visiwa vya Tiran na Sanafir yameidhinishwa na Ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni. Wizara za vita na mambo ya nje za utawala huu pia zimeidhinisha makubaliano hayo.
Hapo awali iliripotiwa kwamba kwa vile Saudi Arabia na utawala ghasibu wa Israel hazina uhusiano wa kidiplomasia, haziwezi kuwa na makubaliano ya moja kwa moja ya pande mbili katika visiwa hivyo viwili vilivyotajwa, na Misri na Marekani zinatafuta suluhu za kimahakama na kidiplomasia ili kukamilisha makubaliano hayo.
Kwa mujibu wa makubaliano ya Camp David kati ya Misri na Israel, Misri imejitolea kuzipokonya silaha Tiran na Sanafir na kukubaliana na ombi la Tel Aviv la kutumwa waangalizi wa kimataifa chini ya amri ya Marekani katika visiwa hivi.
Saudi Arabia ilikabidhi udhibiti wa visiwa hivi viwili, ambavyo ni lango la bandari za Aqaba na Eilat, kwa Misri mwaka 1950. Sasa mashauriano ya pande tatu yanaendelea ili kurudisha umiliki wa visiwa hivi kwa Saudi Arabia.
Licha ya maandamano ya umma nchini Misri, bunge la nchi hiyo mwezi Juni 2017 na Mahakama ya Juu ya Misri mwezi Machi 2018 ziliidhinisha makubaliano ya kuhamisha umiliki na mamlaka ya visiwa hivi viwili hadi Saudi Arabia; Lakini makubaliano haya pia yalihitaji ridhaa na idhini ya utawala wa Kizayuni kutokana na maafikiano ya mwaka wa 1979.