Serikali ya Saudi Arabia imewatia mbaroni maafisa 78 wa serikali kwa tuhuma za ufisadi, kula rushwa, utapeli, kutakatisha fedha na kutumia vibaya madaraka yao.
Taasisi ya kupambana na ufisadi nchini Saudi Arabia, kwa miaka kadhaa sasa imekuwa ikichunguza kesi nyingi za ubadhirifu na ufisaidi na hadi hivi sasa mamia ya wafanyakazi wa hivi sasa na wa zamani wa sekta mbalimbali wametiwa mbaroni kwa ufisadi, kula rushwa na kutumia vibaya madaraka yao. Wamo pia wananchi wa kawaida na hata wageni.
Shirika la habari la Tasnim limeinukuu taasisi hiyo ya kupambana na ufisadi ya Saudi Arabia ikisema kuwa, wafanyakazi 78 waliotiwa mbaroni hivi sasa ni kutoka wizara za ulinzi, afya, mahakama, manispaa za miji, wakuu wa vijiji na sekta ya nyumba. Wote wamekamatwa kwa kula rushwa, kutumia vibaya madaraka, utapeli na utakatishaji fedha.
Mwaka 2017, mfalme wa Saudia, Salman bin Abdul Aziz alitoa amri ya kuundwa taasisi ya kupambana na ufisadi chini ya uongozi wa mwanawe Mohammad bin Salman ambaye ndiye mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia. Tangu wakati huo hadi hivi sasa makumi ya watu wa ukoo wa kifalme na viongozi wa hivi sasa na wa zamani wa serikali wametiwa mbaroni kwa tuhuma hizo za ufisadi.
Wimbi jipya la kutiwa mbaroni maafisa wa serikali ya Saudia Arabia kwa ubadhirifu wa fedha na kupokea rushwa linashuhudiwa hivi sasa katika hali ambayo, maafisa wa nchi hiyo hawajatoa ufafanuzi wa kina ni mambo hasa yaliyopelekea kutiwa mbaroni watu hao.