Makumi ya watu wafariki dunia katika mlipuko nchini Bangladesh

Moto na mlipuko mkubwa umesababisha vifo vya takriban watu 40 baada ya vifo 8 kuongezeka na mamia ya wengine kujeruhiwa kwenye ghala moja lililoko karibu na mji wa Chittagong nchini, Bangladesh.

Mamia ya watu walifika katika eneo hilo kukabiliana na moto huo wakati makontena kadhaa yalipopuka katika eneo la Sitakunda.

Mamlaka husika zinasema kuwa, chanzo cha moto huo bado hakijajulikana, lakini inadhaniwa kuwa kemikali zilihifadhiwa katika baadhi ya makontena hayo. Hospitali katika eneo hilo zimezidiwa na zimeomba kuchangia damu. Wengi wa waliojeruhiwa wanaripotiwa kuwa katika hali mbaya huku majeraha ya moto yakichukua asilimia 60 hadi 90 ya miili yao.

“Mlipuko huo ulinirusha umbali wa mita 10 kutoka mahali nilipokuwa nimesimama. Mikono na miguu yangu imeungua,” dereva wa lori Tofael Ahmed aliziambia duru za habari.

Mhudumu mwingine wa kujitolea aliwaambia wanahabari kwamba, ameona miili zaidi ndani ya eneo lililoathiriwa na moto huo.

Wazima moto kadhaa ni miongoni mwa waliouawa na kujeruhiwa katika mkasa huo wa ajali ya moto. Bohari hiyo ilikuwa na nguo za mamilioni ya dola zilizokuwa zikisubiri kusafirishwa kwa wauzaji reja reja wa nchi za Magharibi, kulingana na afisa wa serikali ya eneo hilo. Bangladesh ni muuzaji mkuu wa nguo kwa nchi za Magharibi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *