Malalamiko ya Wapalestina dhidi ya kuyahudisha mfumo wa elimu wa Quds

Skuli za Palestina katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu zimeanzisha mgomo jumuishi kwa ajili ya kulalamikia sera za elimu za utawala ghasibu wa Israel pamoja na mpango mchafu wa utawala huo wa kuziyahudisha shule za Kipalestina.

Moja ya mikakati michafu ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina ni kufuta utambulisho wao strajia hii ya Israel imekuwa ikitekelezwa katika kalibu kama kuharibu na kubomoa nyumba za Wapalestina, ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi, kuendelea kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kubadilisha utambuulisho wa kidini wa wananchi wa Palestina ambao ni Uislamu.

Katika miaka ya hivi karibuni na ukiungwa mkono na Marekani, utawala ghasibu wa Israel uliitangaza Quds kuwa eti mji mkuu wake. Hivi sasa pia Israel inafanya njama za kuliweka hilo pia katika vitabu vya masomo vya Wapalestina wanaoishi Beitil-Muqaddas na hivyo kuutambulisha mji huo kama mji mkuu wa Israel. Moja ya vitabu vya masomo ambacho kimeandaliwa kwa ajili ya mwaka mpya wa masomo ndani yake Wazayuni wameutambulisha mji wa Quds katika vitabu vya Kiarabu kuwa mji mkuu na mji mkubwa zaidi wa Israel. Hatua hii kwa hakika inakinzana wazi na ukweli wa historia na bila shaka imechukuliwa katika fremu ya muendelezo wa kuziyahudisha ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Fauka ya hayo, katika vitabu hivyo vya masomo vya Wapalestina wa Quds, utawala vamizi wa Israel umechukua hatua ya kufuta taarifa, nembo na alama za kihistoria na kidini za Wapalestina na badala yake kuzipachika nembo za Kiyahudi.

Siyo hayo tu, bali katika vitabu hivyo vipya vya masomo kumefanyika njama za kuzipigia debe na kuzitambulisha sherehe na maadhimisho ya Kiyahudi huku nembo na athari za Kiislamu, Kiarabu na Kikristo zikiporwa na kufumbiwa macho. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamepiga marufuku kufanyika shughuli yoyote ya kitaifa kama vile kutundika bendera ya Palestina katika shule za Palestina au kufundisha wimbo wa taifa wa Palestina katika skuli hizo.

Lengo kuu la hatua hizi za Wazayuni ni kufuta utambulisho wa Kipalestina na badala yake kuufanya mfumo wa kielimu wa skuli za Wapalestina kuwa ni wa Kiyahudi. Kwa maneno mengine ni kuwa, utawala wa kibaguzi wa Israel sanjari na kubadilisha utambulisho katika kalibu ya sera zake za kivamizi, unafanya kila uwezalo kuyaingiza mabadiliko hayo katika mfumo wa elimu na vitabu vya masomo na hivyo kuyafanya hayo kuwa sehemu ya utamaduni wa Wapalestina.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana harakati na makundi ya kisiasa ya Palestina huko Quds yametoa taarifa yakilalamikia sera bandia na haramu za kielimu za utawala dhalimu wa Israel za kutaka kuchomeka na kuingiza kwa nguvu mambo ya Kiyahudi katika vitabu vya masomo vya Wapalestina huko Quds. Makundi hayo yanasisitiza kwamba, hayakubaliani na njama za Israel za kubadilisha mfumo wa elimu huko Quds na hivyo wataanzisha mgomo wa umma kulalamikia hilo.

Muungano wa Walimu wa Palestina umetangaza mfungamano wao na shule za Quds katika kuitisha mgomo na kueleza bayana kwamba, wanafunzi, walimu, wafanyakazi na maafisa wengine wa idara ya elimu na mafunzo hawatahudhuria shuleni wakilalamikia muhtawa wa mfumo huo wa elimu.

Kabla ya hapo, Kamati ya Masuala ya Wanafunzi ya Chuo cha Ibrahim huko Quds ilikuwa imeonya kuhusiana na hujuma ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya ratiba na mitaala ya masomo ya skuli za serikali hususan huko Quds inayokaliwa kwa mabavu na kutangaza kuwa, skuli hizo zinakabiliwa na hatari ya maamuzi ya kidhalimu ya utawakla vamizi wa Israel unaotaka kutwisha mbinu za ufundishaji ambazo kimsingi ni za upotoshaji mambo.

Israel ikiwa na lengo la kukabiliana na malalamiko na upinzani huu na wakati huo huo kutwisha sera zake za kielimu imetishia kwamba, endapo walimu na maafisa elimu wa shule za Palestina watakataa kuingia madarasani na kutokubali kufuata mtaala huo wa masomo, basi itavuruga bajeti ya shule hizo. Chuo cha Ibrahim nacho kimetishiwa kufutiwa usajili na kufungwa endapo kitakataa kufuata mfumo huo mpya wa ufundishaji. Wizara inayotambulika kwa jina la Maarifa ya utawala wa Kizayuni nayo ilitangaza hivi karibuni kwamba, itazishinikiza skuli za Quds ili zifuate maagizo yake na kulifanya hilo kama sharti la kupatiwa shule hizo msaada wa fedha. Utendaji huu wa utawala ghasibu wa Israel unaonyesha kuwa, utawala huom umeanzisha duru mpya ya kukabiliana na Wapalestina lakini mara hii katika fremu ya hujuma za kielimu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *