Maldives kuwapiga marufuku Waisraeli kuingia nchini humo

Maldives imetangaza kuwa itawapiga marufuku wenye paspoti za utawala haramu wa Israel kuingia katika visiwa hivyo vinavyopatikana katika Bahari ya Hindi.

Serikali ya Jamhuri ya Maldives imesema inaandaa sheria ya kuwapiga marufuku Waisraeli kuingia katika nchi hiyo ndogo ya Asia Kusini, ambayo aghalabu ya wakazi wake ni Waislamu.

Msemaji wa Ofisi ya Rais Mohamed Muizzu wa nchi hiyo amesema, “Rais ameazimia kuzipiga marufuku pasi za kusafiria za Israel.” Hata hivyo hajatoa maelezo ya kina kuhusu tarehe ya kuanza kutekelezwa marufuku hiyo.

Serikali ya Maldives imechukua hatua hii kufuatia malalamiko na ghadhabu za wananchi wa visiwa hivyo juu ya jinai za kutisha zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Wananchi wa mataifa mbali mbali duniani yakiwemo ya Magharibi wamekuwa wakiandamana kuonyesha mshikamano na uungaji mkono kwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, ambao wanakabiliwa na vita vya mauaji ya kimbari vya utawala dhalimu wa Israel.

Kadhalika Rais Muizzu wa Maldives ametangaza kuanzisha kampeni ya kitaifa ya kuwachangishia pesa wananchi madhulumu wa Palestina. Mpango huo wa taifa zima unafanyika chini ya kaulimbiu ya “Wamaldives katika Mshikamano na Wapalestina.”

Takriba Waisraeli 11,000 waliitembelea Maldives mwaka jana, hiyo ikiwa ni asilimia 0.6 ya watalii wote waliovitembelea visiwa hivyo vya Bahari ya Hindi 2023.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *