Baada ya hivi karibuni kuzuka vurugu na machafuko mapya nchini Iran maadui sugu wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu walichukua hatua ya kufuatilia senario ya kuligawa taifa hili katika kambi mbili.
Katika senario hii, maadui wamejikita katika masuala mbalimbali. Senario hii kubwa inagawanywa pia katika nyuga nyingine ndogo zaidi mithili ya kikosi cha polisi, utawala, raia, mamlaka. kaumu na vilevile Ushia na Usuni. Kwa msingi huo, swali linaloulizwa ni kuwa, lengo la maadui la kujikita katika suala la utambulisho wa kitaifa na kuleta utambulisho pacha ni nini?
Kuhusiana na hili inawezekana kuashiria nukta kadhaa muhimu.
. Lengo la Kwanza: Kuzusha mpasuko wa kijamii ndani ya jamii ya Iran
Inaonekana kuwa, lengo la kwanza la kuleta utambulisho wa aina mbili ni kuzusha mpasuko wa kijamii nchini Iran. Mpasuko wa kijamii maana yake ni kuibadilisha jamii moja yenye mshikamano na kuifanya kuwa jamii iliyosambaratika na ya vipande vipande. Hii ina maana ya kuulenga na kuuandama umoja na mshikamano wa kijamii. Jamii ambayo itakumbwa na hali hii basi kuibuka machafuko na ukosefu wa amani ni jambo linalowezekana kama ambavyo katika miezi miwili iliyopita mijiji kadhaa ya Iran ikiwemo ya Shiraz, Izeh na Isfahan kulishuhudiwa mashambulio ya kigaidi. Kadhalika jamii ambayo inataabika kwa kuweko mpasuko na tofauti za kimatabaka, katu haiwezi kupiga hatua katika njia ya ustawi na maendeleo na kimsingi itakumbwa na mapaganyiko wa kijamii na kisiasa.
. Lengo jingine: Kudhoofisha rasilimali watu
Lengo la pili muhimu katika kuleta utambulisho pacha, ni kudhoofisha rasilimali watu katika nchi. Maadui na watu wenye chuki dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya katika miaka ya hivi karibuni wamefanya njama lukuki, mtawalia na nyingi kwa lengo la kudhoofisha rasilimali watu hapa nchini. Siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa za serikali ya iliyopita ya Marekani ya Donald Trump zilifuatiliwa pia kwa lengo hili hili. Filihali, kudhoofisha na kuharibu rasilimali watu ndio mhimili wa vita laini (soft war) na vita vya vyombo vya habari vinaendeshwa na maadui. Lengo hili muhimu huko nyuma lilikuwa likifuatilia katika kalibu yya masuala ya kiuchumi na hii leo linafuatilia katika mhimili wa utambulisho.
. Kuikwamisha serikali katika uga wa kimataifa
Moja ya malengo ya senario ya kuleta utambulisho pacha ni kuifanya serikali kutokuwa na utendaji katika uga wa kimataifa. Licha ya kuwa, mazungumzo baina ya Iran na madola ya Magharibi yamesimama katika miezi ya hivi karibuni, lakini kumekuweko na mabadiliko ya barua na jumbe baina ya pande mbili. Baadhi ya ripoti zinaeleza kuwa, madola ya upande wa pili wa mazungumzo na Iran na vilevile serikali ya Marekani yanataka Tehran iweke kando na kufumbia macho matakwa yake. Sababu ya takwa hilo ni vurugu na machafuko yaliyoibuka hivi karibuni. Madola hayo yanaamini kuwa, kuendelea vurugu na machafuko ni fursa nzuri ya kuishinikiza serikali ya Iran na kuifanya ilegeze kamba katika baadhi ya mambo katika mazungumzo ya nyuklia. Hata hivyo njama hizo zinaonekana kugonga mwamba, kwani hadi sasa Iran haijawa tayari kulegeza kamba hata kidogo.
. Kutilia shaka uhalali wa mfumo
Lengo kuu la njama za maadui ni kuzithibitishia fikra za umma ndani ya nchi na fikra za walimwengu kwamba, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unakabiliwa na mgogoro wa uhalali. Kimsingi hasa lengo lao ni kuanzisha vita vya kisaikolojia, kifikra na vya utambuzi vinavyojulikana kwa kimombo kama “Cognitive Warfare” dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, na hivyo kuibua mgogoro wa uhalali wa mfumo unaotawala hapa nchini. Katika vita hivi lengo kuu ni kuwafanya wananchi kutokuwa na imani na mfumo unaotawala.
Mapinduzi ya Kiislamu ni mfumo uliotokana na azma na irada pamoja na matakwa ya wananchi. Hata hivyo adui kwa kuibua utambulisho pacha na hususan kuutenganisha utawala na wananchi anafanya njama za kutilia shaka na alama ya swali uhalali wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Ili kufikia lengo hili, maadui wanatumia mbinu mbalimbali na wamejikita zaidi katika kutumia teknolojia na vyombo vya mawasiliano kusema uongo, kudhibiti fikra na kuja na simulizi za urongo na bandia ambapo walengwa wakuu katika hili ni tabaka la vijana.
Katika hili maadui hujaribu kutumia mbinu tofauti kuwakinaisha vijana na kuwafanya wakane mafanikio yote yaliyoletwa na mfumo sambamba na kupuuza maendeleo na ustawi uliopo. Hatua inayofuata ni kuzalisha hasira, ghadhabu na chuki za wananchi dhidi ya mfumo sambamba na kuleta mgogoro wa uhalali wa serikali iliyoko madarakani, kwani kinyume na hivyo, adui hatoweza kufikia malengo yake katika njia hii.