Malengo ya pamoja ya Aal-Khalifa na Israeli kuhusu safari ya Herzog mjini Manama

Isaac Herzog, mkuu wa utawala wa Kizayuni unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu, aliwasili nchini Bahrain tarehe 4 Disemba kwa ziara rasmi ambapo alikutana na kuzungumza na Mfalme Hamad bin Issa wa nchi hiyo. Safari hiyo imefanyika kwa mwaliko rasmi wa mfalme huyo.

Isaac Herzog alitangaza mapema Jumamosi kwamba alikuwa amepanga kuelekea Manama kwa mwaliko wa Hamad bin Issa Aal Khalifa. Kwa hivyo swali ni je, ni kwa nini mfalme wa Bahrain amemwalika rais wa utawala wa Kizayuni kutembelea Manama?

Inaonekana kwamba sababu ya kwanza ya Al-Khalifa kumualika kiongozi huyo wa Kizayuni katika nchi hiyo ndogo ya Kiislamu ni kufidia mapungufu ya uhalali wa utawala wake kwa kupanga safari za nje. Kwa hiyo, kabla ya kufanyika uchaguzi wa hivi karibuni huko Bahrain, mfalme huyo alimwalika Papa Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, kutembelea Manama, na baada ya uchaguzi, amekuwa mwenyeji wa rais wa utawala wa Kizayuni. Hatua ya utawala wa Aal-Khalifa ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Wazayuni inaweza kuchukuliwa kuwa kielelezo cha mgogoro uliopo kati ya utawala huo na watu wake.

Jambo la pili ni kwamba utawala wa al-Khalifa unataka kuonyesha kuwa unafuatilia kuimarisha mazungumzo kati ya dini tofauti. Utawala huo huku ukiwa unawakandamiza Mashia wa Bahrain, unajaribu kuonyesha kuwa unawatetea Wakristo na Mayahudi na ndio maana ukaamua kuwaalika Papa na Herzog kutembelea nchi hiyo.

Jambo la tatu ni kuwa, serikali ya Bahrain inajaribu kuimarisha usalama wake kupitia upanuzi wa uhusiano na utawala wa Kizayuni. Ni kwa msingi huo ndipo upinzani wowote dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Bahrain ukakabiliwa na ukanadamizaji mkubwa.

Abdul Hadi al-Khawaja, mwanaharakati wa kisiasa wa Bahrain alikamatwa na kutupwa korokoroni kwa tuhuma za “kutukana serikali ya kigeni”, ambayo ni Israel. Kabla yake, Mai bint Mohammad al Khalifa, kutoka ukoo unaotawala huko Bahrain, aliondolewa kwenye nafasi ya mkuu wa Jumuiya ya Utamaduni na Mambo ya Kale ya Bahrain kwa kutompa mkono Eitan Na’eh, balozi wa utawala wa Kizayuni huko Manama.

Lakini je, utawala wa Kizayuni una malengo gani kuhusiana na ziara ya Herzog nchini Bahrain?

Moja ya malengo ya ziara ya Herzog huko Bahrain ni kuimarisha uhusiano na nchi hiyo. Bahrain ilianzisha mwenendo wa kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel mwaka 2020, ambapo uhusiano huo umekuwa ukiboreka katika miaka miwili iliyopita.

Hata hivyo, lengo muhimu zaidi la safari ya mkuu wa utawala wa Kizayuni nchini Bahrain na kisha Imarati ni kuonesha kuwa utawala huo hauchukiwi katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu. Wakati wa michezo ya Kombe la Dunia huko Qatar, raia wa nchi tofauti za Kiarabu sio tu walikataa kuzungumza na vyombo vya habari vya Israel, bali waliunga mkono wazi wazi taifa la Palestina, na hata mchezaji wa Morocco Jawad Elyamiq alinyanyua bendera ya Palestina na kuiweka begani baada ya ushindi wa Morocco dhidi ya Canada na kufanikiwa nchi hiyo kuingia katika hatua ya maondoano. Herzog amesafiri Bahrain wakati wa Kombe la Dunia la Qatar na kisha kwenda Imarati ikiwa ni katika juhudi za kujaribu kuthibitisha kwamba utawala wa Kizayuni hauchukiwi katika eneo.

Herzog anataka kufikia lengo hilo huku katika siku za hivi karibuni kukiwa kumefanyika maandamano mengi ya wananchi wa Bahrain ya kupinga safari yake hiyo na suala la kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala huo, suala ambalo limepelekea kuimarishwa hatua za kiusalama wakati wa kufanyika safari yake huko Manama.

Sheikh Issa Qassim, kiongozi wa kidini wa mapinduzi ya Bahrain ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kama tunavyonukuu: “Kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni ni hiana, na kuchafuliwa ardhi ya Bahrain kwa safari ya kuchukiza ya rais wa utawala wa Kizayuni ni fedheha ambayo taifa letu tukufu haliikubali.”

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *