Malkia Elizabeth II wa Uingereza aliyeitawala nchi hiyo ya Ulaya kwa muda wa miaka 70 amefariki dunia Alhamisi akiwa na umri wamiaka 96 huku mustakabali wa ufalme anaouacha ukiwa matatani.
Masaa machache kabla ya kifo chake, kasri ya Buckingham ilikuwa imetoa taarifa ikieleza wasiwasi juu ya afya ya Malkia huyo baada ya kufanyiwa tathmini ya afya yake
Mwanawe Charles, sasa ndiye mfalme na atakuwa mkongwe zaidi kuwahi kuchukua nafasi ya Ufalme wa Uingereza kwani ana umri wa miaka 73.
Malkia Elizabeth ameaga dunia katika nyumba yake ya Balmoral huko Scotland, eneo ambalo watu wake wengi wanataka kujitenga na Uingereza na kuunda nchi huru.
Barani Afrika Malikia Elizabeth II anakumbwa kwa jinai ambazo utawala wa kikoloni ulitenda katika nchi ambazo zilikuwa zinapigania uhuru. Kwa mfano askari wa kikoloni chini ya amri ya Malkia Elizabeth walitenda jinai na kuwaua maelfu ya wapigania ukombozi wa Kenya hasa wapiganaji wa kundi la Mau Mau.
Hivi karibuni tu watu zaidi ya 100,000 kutoka koo ya Talai katika Kaunti ya Kericho nchini Kenya, walimwandikia barua mwanamfalme William wa Uingereza, kutaka waombwe radhi, kufuatia mateso waliyopitia na kuporwa ardhi zao zenye rotuba wakati wa kipindi cha ukoloni kabla ya kupata uhuru mwaka 1963.
Malikia Elizabeth pia ameacha familia ya kifalme ambayo katika miaka ya hivi karibuni imekumbwa na kashfa chungu nzima.
Hivi karibuni ilifichuka kuwa, Charles, ambaye sasa ni Mfalme wa Uingereza, alikubali mchango wa pauni milioni 1 ($ 1.19 milioni, euro milioni 1.21) kutoka kwa familia ya gaidi aliyeuawa wa Saudia, Osama bin Laden.
Charles aliripotiwa pia kukubali michango mingine yenye utata kutoka kwa mwanasiasa wa Qatar ambapo pesa taslimu zilizotolewa kutoka 2011 hadi 2015 zilipokewa zikiwa kwenye mifuko.
Aidha Kuanzia miaka ya 1970 hadi 90, Charles na Camilla Parker Bowles walikuwa kwenye uhusiano nje ya ndoa wakati Charles tayari alikuwa na mke. Mwishowe uhusiano huo haramu ulimpelekea Malkia Elizabeth kumlazimisha Charles ampe talaka Diana.
Kashfa nyingine kati ya nyingi ni wakati mtoto wa pili wa Malkia Elizabeth, Mwanamflame Andrew alipomtumia msichana mdogo kama mtumwa wa ngono.
Kasri ya Buckingham awali lilijaribu kutetea “heshima” ya Andrew na kuzima habari zilizoenea katika uwanja huo. Pamoja na hayo, ukweli ulipodhihiri wazi, Andrew alivuliwa vyeo vyake vyote na Malkia.
Kufuatia kifo cha Malikia Elizabeth, mustakabali wa familia ya kifalme Uingereza uko matatani kwani watu wengi nchini Uingereza wamekuwa wakilalmika kuwa familia hiyo inawasababishia walipa kodi hasara.