Mamia ya watu wamekusanyika katika mji mkuu wa Senegal Dakar kutaka uchaguzi wa rais wa nchi hiyo ufanyike kabla ya Aprili 2, tarehe ambayo ndipo unapomalizika muhula wa rais wa hivi sasa, Macky Sall
Nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika Magharibi ilitumbukia kwenye mgogoro wa kisiasa tarehe 3 mwezi uliopita wa Februari wakati Macky Sall alipoakhirisha uchaguzi wa rais uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 25.
Hatua hiyo ililaaniwa na wapinzani kuitwa ni mapinduzi ya katiba, na ilizusha maandamano makubwa ambayo yamesababisha vifo vya watu wanne.
Hatimaye Baraza la Katiba lilitengua hatua hiyo ya Rais Sall na tangu wakati huo Senegal imekuwa ikingojea tarehe mpya ya uchaguzi.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Februari pia, wagombea wengi katika uchaguzi ulioakhirishwa nchini Senegal na kundi kubwa la vyama na asasi za kiraia kwa pamoja walisema kuwa, hawatashiriki katika mazungumzo yaliyopendekezwa na Rais Macky Sall ya kuamua tarehe ya upigaji kura ambao aliuakhirisha mwanzoni mwezi huo wa Februari.
Mwito wa kumtaka Sall atangaze siku ya uchaguzi wa rais baada ya kuuakhirisha ghafla uchaguzi wa Februari 25 na kusababisha mgogoro wa kisiasa kwa wiki kadhaa umekuwa ukiongezeka siku baada ya siku.
Tayari Macky Sall ametangaza kuwa, ataachia madaraka ifikapo Aprili Pili wakati ambapo muda wake wa uongozi utakuwa umemalizika. Hata hivyo hadi hivi sasa kiongozi huyo hajatangaza tarehe mpya ya uchaguzi huko Senegal.
Wagombea 15 kati ya 20 walioidhinishwa kugombea katika uchaguzi wa urais wa Senegal wametaka uchaguzi mpya uwe umeshafanyika kabla ya tarehe Pili Aprili.