Serikali ya Sudan imetangaza kwamba, makadirio yanaonyesha kuwa karibu raia milioni tano wa mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum, na maeneo mengine wameyakimbia makazi yao.
Katika mahojiano yake na kampuni ya Sputnik, Sadiq Hassan Farini, Waziri wa Ustawi wa Jamii wa Sudan ametangaza kuwa, kuendelea kwa mapigano nchini Sudan kumezidisha hali mbaya ya uchumi na kuongeza kiwango cha umaskini kuliko hapo awali.
Ferini ameongeza kuwa: Kiwango cha umaskini kinakadiriwa kuwa karibu 80%, na kitazidisha maradufu uwajibikaji wa kijamii wa serikali katika siku zijazo baada ya kumalizika vita vya sasa.
Hapo awali, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi alitangaza katika taarifa yake kwamba watu milioni sita nchini Sudan wako umbali wa hatua moja tu kutumbukia kwenye baa njaa. Alisema, zaidi ya watoto milioni 14 wa Sudan wanahitaji msaada wa kibinadamu na kwamba jamii ya kimataifa inapaswa kuingilia kati kumaliza vita nchini Sudan.
Umoja wa Mataifa pia umeonya kuwa mamilioni ya watu nchini Sudan wanakabiliwa na uhaba wa chakula na baadhi yao wanaaga dunia kutokana na ukosefu wa huduma za matibabu.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji pia limetangaza kuwa, tangu kuanza kwa mapigano ya ndani kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), zaidi ya Wasudani milioni moja wamekimbia nchi jirani.