Kati ya mataifa ya Kiarabu ya Ukanda wa Ghuba ya Uajemi, Oman ni moja ya mataifa ambayo daima yamekuwa na uhusiano thabiti na wa kirafiki na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Taifa la Oman daima limefanya juhudi za kuwa mpatanishi katika masuala yanayohusiana na migogoro ya eneo la Asia Magharibi.
Uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ufalme wa Oman una umuhimu mkubwa na wa aina yake hasa kwa kutilia maanani kuwa jirani mataifa haya mawili na Lango Bahari la Kistratejia la Hormoz sambamba na kuweko mashirikiano ya kiutamaduni, kidini na ya kihistoria. Aidha uhusiano rasmi wa kidiplomasia baina ya mataifa haya mawili ulianza rasmi tarehe 23 Agosti1971 kwa kutolewa taarifa ya pamoja. Katika kipindi cha kabla ya Mapinduzi ya Kislamu ya Iran na katika hatua mbalimbali baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1978, nchi hizi kila moja ilipokea kwa mikono miwili suala la kupanuliwa na kustawishwa zaidi uhusiano baina ya pande mbili na hakujawa na kadhia maalumu ambayo imepelekea uhusiano huo kukumbwa na hali ya mgogoro au kuzorota.
Mwaka 1979 kutumwa kikosi cha kijeshi cha Iran huko Oman kwa ajili ya kuunga mkono utawala wa Sultan Qaboos katika vita vya Dhofar na kukabiliana na waaasi waliokuwa wakipigania kujitenga kulipelekkea kulindwa umoja na mshikamano wa nchi hiyo ya Kiarabu.
Operesheni ya kijeshi ya jeshi la Iran katika vita vya Dhofar ilikuwa na mchango mkubwa katika kubadilika hali ya mambo kwa maslahi ya utawala wa Sultani wa Oman na kusambaratishwa wapinzani kiasi kwamba, kubakia madarakani Sultani Qaboos pamoja na utawala wake kuwa mdaiwa wa Iran.
Kuanzia wakati huo ambapo Oman ilidiriki umuhimu wa jirani yake mkubwa yaani Iran, ikaonyesha kuwa na mkakati thabiti katika uhusiano na majirani zake ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu.
Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana baada ya vita vya kichokozi vilivyoanzisha na Iraq dhidi ya Iran, ikatanguliza mbele sera za kutaka maridhiano zaidi katika uhusiano na Tehran. Agosti 2010 Oman na Iran zikatiliana saini mkataba wa usalama baina yao.
Kwa miaka msingi Oman imekuwa ikifuata mkondo wa siasa za udiplomasia wenye msingi wa amani na kutoegemea upande wowote na ndio maana inatambulika kama mpatanishi mzuri. Licha ya Oman kuwa katika eneo la kijiografia ambalo ni nyeti na lenye mizozo na mivutano, lakini nchi hii imeweza kuwa mbali kwa makumi ya kilomita na sokomoko, mivutano na mizozo na hata imefanikiwa mara chungu nzima kucheza vyema nafasi ya upatanishi kwa majirani zake.
Katika muongo wa 80 Hijria Shamsia, Oman iligeuka na kuwa mlindaji wa maslahi ya Iran nchini Uingereza na baadaye Canada. Mwaka 2005, sio tu kwamba, Oman ilikuwa na mchango mkubwa katika mazungumzo kuhusiana na wafungwa wasio wa Kiirani kama mabaharia 12 wa Uingereza na wapanda milima watatu wa Kimarekani, bali ilifanikiwa mara chungu nzima kufanikisha kuachiliwa huru wafungwa wa Kiirani katika mataifa mengine.
Katika miaka ya hivi karibuni pia, daima Oman imekuwa mmoja wa wapatanishi wakuu baina ya madola ya Magharibi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan katika mazunguumzo ya nyuklia. Mwaka 2011, Waziri wa wakati huo wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani John Kerry alianzisha juhudi za kuhakikisha kunakuweko mazungumzo ya ana kwa ana baina ya Iran na Marekani na akaitaka serikali ya Oman iwe mpatanishi katika mazungumzo hayo. Juhudi hizo zilipelekea mwaka 2012 kufanyike baadhi ya mikutano katika mji mkuu wa Oman, Muscat na hatimaye mwaka 2014 kikao cha kwanza cha maafisa wa Iran na Marekani kikafanyika rasmi nchini Oman.
Licha ya kuwa uhusiano wa kibiashara baina ya Iran na Oman sio mbaya na katika uga wa ubalishanaji biashara, Oman inashika nafasi ya sita miongoni mwa mataifa jirani yanayoshirikiaina na Iran na katika Ghuba ya Uajemi inashika nafasi ya pili, lakini kwa vyovyote itakavyokuwa uhusiano huu haujaenda sambamba na uhusiano wa kisiasa na takwimu zinaonyesha kuwa, hakujatumiwa suhula na uwezo uliopo baina ya pande mbili kama inavyotakiwa kwa ajili ya kupanua uhusiano wa kiuchumi.
Hapana shaka kuwa, uhusiano wa Iran na Oman hauishi katika suala la kuwa ni majirani tu, bali kuna mambo mengi ambayo ni ya pamoja baina ya mataifa haya mawili hasa katika uga wa kidini na kiitikadi ambayo ni ya karne nyingi.
Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana katika safari yake ya hivi karibuni huko nchini Oman, Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akabainisha kwamba, Tehran na Muscat zina mambo mengi zinayoshirikiana iwe ni ya pande mbili, kieneo au kimataifa.