Mapitio ya mkutano wa kwanza wa ushirikiano wa kiuchumi wa Iran na mataifa ya Afrika magharibi

Katika siku ya kwanza ya mkutano wa ushirikiano wa kiuchumi wa Iran na mataifa ya Afrika magharibi kumetiwa saini hati 20 za ushirikiano katika nyuga tofauti zikiwemo za kisiasa, kiuchumi, kibiashara na kiutalii.

Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano wa Sayansi na Uchumi baina ya Iran na nchi za Afrika magharibi ulianza jana Jumatatu hapa mjini Tehran. Mawaziri, mabalozi, na wawakilishi wa sekta za biashara, nishati na viwanda wa Iran na nchi za Afrika Magharibi wanashiriki katika mkutano huo wa siku tatu.

Mohammad Mokhber, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kusainiwa hati 20 za ushirikiano katika nyuga tofauti zikiwemo za kisiasa, kiuchumi, kibiashara na kiutalii katika siku ya kwanza ya mkutano huo baina ya Jamhuri ya Kiislamu na mataifa hayo ya Afrika kunaonesha azma na irada thabiti ya kisiasa ya pande mbili ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina yao.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, serikali ya awamu ya 13 ya Rais Ebrahim Raisi itafanya kila iwezalo kukuza na kustawisha zaidi ushirikiano wake na mataifa ya Kiafrika.

Amebainisha kuwa, mabadilishano ya kibiashara baina ya Iran na nchi za Afrika magharibi yanaunda asilimia 40 ya biashara zote baina ya Iran na bara la Afrika, na kwamba kuna haja ya kunyanyua juu zaidi kiwango hicho.

Ukweli wa mambo ni kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan serikali ya awamu ya 13 chini ya uongozi wa Ebrahim Raisi imekuwa ikitoa kipaumbele katika sera zake za nje juu ya suala la kuimarisha uhusiano wake na mataifa mengine husuusan ya Kiafrika na kusukuma mbele guruumu la sera za kigeni zenye uwiano. Katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, Tehran imetangaza mara chungu nzima kwamba, inalipa kipaumbele suala la kuwa na ushirikiano na mahusiano mazuri na mataifa ya Kiafrika. Katika kipindi hiki jumbe mbalimbali za kiuchumi kutoka katika mataifa ya Kiafrika kama Nigeria, Ivory Coast, Kenya, Tanzania, Cameroon, Senegal, Guinea na Mali zimetembelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Aidha takwimu zinaonyesha kuongezeka kwa mahusiano ya kibiashara ya Iran na Afrika. Katika kipindi cha miezi minane iliyopita kiwango cha uingizaji na usafirishaji wa bidhaa baina ya Iran na mataifa ya Kiafrika kilifikia dola bilioni 1 na milioni 56. Kiwango hicho ni ongezeko la asimilia 39 ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka uliopita.

Reza Fatemi-Amini, Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Iran ameashiria kukua mabadilishano ya kibiashara baina ya Iran na nchi za Kiafrika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na kueleza juu ya kuongezeka maradufu usafirishaji wa bidhaa za Iran kuelekea barani Afrika.

Pamoja na hayo, kiwango cah biashara kati ya Iran na bara la Afrika ni kidogo, kwani filihali bidhaa zinazoingizwa Iran kutoka Afrika zinakaribia thamani ya dola bilioni 600 huku hisa ya Iran ikiwa haifiki hata dola bilioni mbili. Hii ni katika hali ambayo, kwa upande wa kiuchumi, bara la Aftrika linazingatiwa mno na mataifa ya viwanda ambayo yamekuwa yakihaha kuhakikisha yanawekeza katika bara hilo na hivyo kujidhaminia maslahi yao kupitia utajiri mkubwa wa Afrika.

Kuhusiana na hilo, Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kuashiria udharura wa kustawishwa ushirikiano wa kiuchumi wa Iran na mataifa ya Kiafrika  hususan katika nyuga za nishati, uhandishi, ufundi, usafiri na uchukuzi, kilimo na madini amesema kuwa,  takwimu za sasa za mabadilishano ya kibiashara bainna ya Iran na Afrika haziridhishi hasa kwa kuzingatia uwezo na umuhimu wanaotoa viongozi wa Tehran kwa mataifa ya magharibi mwa Afrika ilitarajiwa kuweko mabadiliko makubwa zaidi ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya pande mbili.

Kwa upande wa kisiasa pia, ni jambo muhimu kustawishwa uhusiano baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mataifa ya Afrika magharibi. Nchi 50 kati ya 55 za Afrika ni wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM na baadhi ya nchi hizo zinakabiliwa na vikwazo. Kadhalika nchi 30 za bara la Afrika ni za Kiislamu huku takribani asilimia 50 ya wakazi wake wakiwa ni Waislamu.

Ni kwa kuzingatia hayo yote ndio maana, weledi wa mambo wanaamini kwamba, kuna kila sababu ya kuimarishwa zaidi uhusiano kati ya Iran na maataifa ya Kiafrika.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *