Katika kuendeleza sera zake za mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon, serikali ya Marekani imewawekea vikwazo watu watatu na makampuni mawili ya Lebanon kwa kisingizio cha kutoa huduma za kifedha kwa harakati hiyo.
Sambamba na hatua zake za kujaribu kupunguza mapenzi na umaarufu wa harakati ya Hizbullah nchini Lebanon, Washington imekuwa kila mara ikiziweka benki na shakhsia wa Lebanon katika orodha yake ya vikwazo kwa madai ya kuwa na uhusiano na harakati hiyo ya muqawama.
Hizbullah ya Lebanon ambayo ni miongoni mwa wadau wakuu wa kambi ya mapambano na muqawama, ina nafasi muhimu na inatoa mchango mkubwa katika kukabiliana na njama na hatua za mhimili wa Kimarekani na Kizayuni katika eneo la Asia Magharibi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, wizara ya fedha ya Marekani ilitangaza jana kuwa, imewawekea vikwazo wahasibu wawili na makampuni mawili ya Lebanon kwa kutoa huduma za kifedha kwa Hizbullah.
Wizara hiyo ya serikali ya Marekani imedai kuwa itamwekea vikwazo pia raia mwingine wa Lebanon kwa kuisaidia Hizbullah kupata silaha.
Hizbullah ni moja ya vyama muhimu vya kisiasa nchini Lebanon.
Hatua hizo za kihasama na kiuadui za Marekani zimeshakosolewa mara kadhaa na wataalamu na wachambuzi wa kisiasa nchini Lebanon ambao wanasema, Hizbullah imekuwa na nafasi muhimu katika kudumisha utulivu na uthabiti nchini humo na katika kupambana na makundi ya kigaidi na yenye misimamo ya kufurutu mpaka katika eneo.