Marekani yazidi kuisaidia UAE katika vita dhidi ya watu wa Yemeni

Ndege za kivita za Marekani aina ya F-22 zimeshuhudiwa zikiwasili katika Kituo cha Ndege za Kivita cha Al-Dhafra siku ya Jumamosi katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Kwa mujibu wa Jeshi la Anga la Marekani, kutumwa kwa ndege hizo za kivita kunafuatia mapatano baina ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin, na Mrithi wa Ufalme wa Abu Dhabi, Mohammed bin Zayed Al Nahyan.

Hatua hiyo inafuatia makubaliano ya pamoja ya kijeshi ya Marekani na UAE yaliyotiwa saini wiki iliyopita. Maafisa wa Marekani hawajatangaza idadi ya ndege za kivita za F-22 zitakazotumwa UAE.

Kwa mujibu wa Gregory Gillot, kamanda wa Kitengo cha Asia Magharibi cha Jeshi la Anga la Marekani, kutumwa kwa wapiganaji hao kutaimarisha uwezo wa kiulinzi wa washirika wa kikanda wa Washington na kutuma ujumbe kwa pande ambazo amedai eti zinahusika katika ‘kukosekana kwa utulivu’ wa kikanda kwamba Marekani na washirika wake wamejitolea katika kile alichosema kuwa eti ni amani na utulivu.

Hatua hiyo inaonekana kuwa ishara ya uungaji mkono kamili wa Marekani kwa UAE, ambayo imekuwa ikilengwa na mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za harakati za mapambano au muqawama wa Yemen. Wanajeshi na wanamapambano wa Yemen wamekuwa wakitekeleza mashambulizi hayo wakilipiza kisasi kwa jinai zinazotekelezwa na muungano vamizi unaaongozwa na Saudia na UAE dhidi ya watu wa Yemen.

Hata hivyo, haijabainika ni kwa namna gani upelekaji wa ndege za kivita za kizazi cha tano za F-22 huko Imarati, ambazo ni maalumu kwa ajili ya kukabiliana na adui mwenye uwezo mkubwa wa ndege za kivita, unaweza kuzuia makombora na ndege zisizo na rubani za Yemen kuendelea kushambulia UAE.

Marekani imekuwa muungaji mkono mkuu wa mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu wakati wa vita vya miaka saba vya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya watu wa Yemen. Licha ya kwamba Rais Joe Biden wa Marekani alitoa ahadi za awali za kushughulikia masuala ya haki za binadamu katika uhusiano na washirika Waarabu wa Washington, lakini kwa hakika hajachukua hatua madhubuti za kuziwekea mashinikizo Saudia na Imarati ili kukomesha mzingiro wa Yemen, bali kinyume chake ameanzisha tena mauzo ya silaha kwa nchi hizo mbili. Katika kampeni yake, Biden alivitaja vita vya Yemen kuwa ni “janga la kimkakati” na kudai kwamba “atakomesha uungaji mkono wa Marekani kwa mashambulizi ya muungano vamizi wa Saudi nchini Yemen, ikiwa ni pamoja na uuzaji wa silaha kwa nchi hiyo.” Hata hivyo, baada ya kuhamia Ikulu ya rais wa Marekani, ameanza sera ya uuzaji wa silaha hatari kwa Saudi Arabia na UAE.

Kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI), Marekani ndiyo muuzaji mkubwa zaidi wa silaha kwa Saudi Arabia na UAE. Utumiaji wa silaha za Marekani kushambulia maeneo ya raia nchini Yemen pia umepelekea kuwibuka ukosoaji kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binadamu.

Amnesty International imesema katika ripoti yake kwamba mashambulizi ya anga ya muungano wa Saudia kwenye jela ya Saada, ambayo yalisababisha vifo vya makumi ya watu, yalitekelezwa kwa kutumia mabomu yaliyotengenezwa  nchini Marekani.

Lynn Maalouf, mtaalamu wa haki za binadamu anasema, “picha za kutisha kutoka Yemen zinaonyesha namna raia wanavyoteseka kutokana na mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia na washirika wake huku mashirika ya  Magharibi yakipata faida kubwa.”

Sambamba na hayo serikali ya Biden inafuata sera ya kulaani mashambulizi ya kulipiza kisasi yanayofanywa na wapiganaji wa Yemen dhidi ya wavamizi wanaotekeleza jinai dhidi ya nchi yao yaani UAE na Saudi Arabia.

Hivi sasa pia Marekani inajaribu kuirejesha harakati ya Ansarullah iliyoko madarakani Yemen katika orodha ya makundi ya kigaidi; hatua iliyochukuliwa na utawala wa zamani wa Marekani katika miezi ya mwisho ya urais wa Donald Trump, ambayo ilifutwa  mwazoni mwa utawala wa Joe Biden.

Bila shaka, hatua ya Washington kupeleka ndege za kivita za F-22 huko UAE inaonyesho kuwa Marekani itaendelea kuwaunga mkono washirika wake wa kikanda. Hatua hiyo imechukuliwa kwa sababu washirika wa kieneo wa Washington hususan Saudi Arabia na Imarati wamekuwa wakitilia shaka azma ya Marekani kuendelea kuwalinda baada ya Washington kuondoka kwa madhila makubwa nchini Afghanistan.

Hata hivyo, hatua hizo za Marekani haziwezi kuzuia oparesheni za Wayemeni za kulipiza kisasi dhidi ya Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *