Mashabiki wa Celtic waunga mkono mapambano ya ukombozi ya watu wa Palestina

Mashabiki wa timu ya kandanda ya Celtic huko Scotland wamebeba na kupeperusha bendera za Palestina katika mechi iliyochezwa jana dhidi ya timu ya Shakhtar Donetsk ya Ukraine, wakitangaza uungaji mkono wao kwa Wapalestina wa eneo la Nablus wanaoendelea kukandamizwa na utawala haramu wa Israel.

Kwa siku ya 16 mfululizo, wanajeshi wa Israel wanauzingira mji wa Nablus huko katika Ukingo wa Magharibi ambako wanavamia na kushambulia ovyo makazi na nyumba za familia za Wapalestina.

Kufuatia hali hiyo, mashabiki wa timu ya Celtic ya Scotland waliohudhuria mechi ya jana kati ya timu hiyo na  Shakhtar Donetsk ya Ukraine, walitoa nara dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel huku wakipeperusha bendera za Palestina katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Mashabiki wa klabu hiyo ya Scotland walipeperusha bendera za Palestina katika dimba la Celtic Park, ambalo lina uwezo wa kuchukua watazamaji zaidi ya 60,000, na kutangaza uungaji mkono wao kwa mapambano ya ukombozi ya Wapalestina hususan katika mji wa Nablus.

Hii si mara ya kwanza kwa mashabiki wa Celtic kuonyesha mshikamano wao na Palestina, na hali kama hii imejikariri mara nyingi katika miaka iliyopita.

Vilevile siku mbili zilizopita, wakati wa mpambano baina ya timu ya Kizayuni ya Maccabi Haifa na PSG katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, mashabiki wa timu ya Ufaransa ya Paris Germain walipiga nara za kuunga mkono mapambano ya Palestina na makazi wa Ghaza.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, wananchi madhulumu wa Palestina wanaendelea kukandamizwa na utawala ghasibu wa Israel kwa zaidi ya miaka sabini. Utawala huo ghasibu unaendelea kufanya jinai na mauaji ya kutisha huko katika ardhi za Palestina kwa himaya na misaada ya hali na mali ya nchi za Magharibi hususan Marekani.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *