Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza, zaidi ya mashabiki 1,300 wa soka wa Uingereza wenye historia ya kufanya vurugu za soka hawataruhusiwa kusafiri hadi Qatar kwa ajili ya kutazama Kombe la Dunia la 2022.
Takwimu mpya za serikali ya London zitaanza kutumika kuanzia Ijumaa ya wiki hii na mashabiki 1,300 wa kandanda watapigwa marufuku kusafiri kwenda Qatar kwa ajili ya kutazama Kombe la Dunia ambapo timu ya taifa ya Uingereza iko katika kundi moja na timu za Marekani, Wales na Iran.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, Suella Braverman amesema: “Hatutaruhusu tabia ya watu wachache wanaovunja sheria kuharibu mashindano ya kusisimua.”
Kwa mujibu wa tangazo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza, mashabiki ambao hapo awali wamesababisha fujo na kuna uwezekano wa kurudia tabia hiyo watapigwa marufuku kusafiri kwenda Doha.
Mamlaka ya Uingereza inasema watu hawa watakabiliwa na faini isiyo na kikomo na kifungo cha miezi 6 ikiwa watajaribu kukwepa sheria.
Mashindano ya 22 ya Kombe la Dunia yatafanyika nchini Qatar kuanzia Novemba 20 hadi Desemba 18.