Mashinikizo ya Israel ya kutaka Afrika Kusini isimamishe mashtaka dhidi yake huko Hague

Utawala wa Kizayuni unalishinikiza Bunge la Marekani Congress, liizuie Afrika Kusini kuendelea na mashtaka dhidi yake Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

Jarida la Marekani la Axios limeandika kuwa, utawala ghasibu wa Israel umeiwekea mashinikizo Congress ya Marekani ili iizuie Afrika Kusini kuendelea na mashtaka yake dhidi ya Tel Aviv katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ.

Tarehe 24 Mei, mwaka huu, Mahakama ya The Hague ilitoa uamusi kuhusiana na kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni kuhusu kufunguliwa vivuko vya misaada katika Ukanda wa Gaza, ambapo iliutaka utawala huo usimamishe operesheni za kijeshi huko Rafah na kufungua vivuko vya nchi kavu vya misaada ya kimataifa kuelekea Gaza.

Afrika Kusini imesema vitendo vya utawala wa Kizayuni huko Gaza ni mfano wa wazi wa mauaji ya halaiki, kwa sababu vita hivyo vinatekelezwa kwa shabaha ya kuangamiza sehemu kubwa ya jamii ya Wapalestina wanaoishi katika ukanda huo.

Kwa mujibu wa Axios, utawala wa Kizayuni wa Israel umezitaka balozi na balozi zake ndogo nchini Marekani kuwasiliana mara moja na wabunge wa serikali kuu ya Marekani, majaji wa Mahakama ya Juu na mashirika ya Kiyahudi kwa ajili ya kuishinikiza Afrika Kusini ibadilishe siasa zake dhidi ya Israel. Utawala wa Israel ulianzisha vita vya mauaji ya umati dhidi ya Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7 mwaka uliopita.

Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza katika takwimu za karibuni kwamba watu zaidi ya elfu 41 wameuawa shahidi na wengine karibu laki moja wamejeruhiwa katika mashambulizi ya jeshi la utawala ghasibu wa Israel katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *