Mashirika 10 ya kutetea haki za binadamu yametangaza himaya na uungaji mkono wao kwa wahanga wa ukandamizaji nchini Saudi Arabia hususan wanaharakati, wafungwa wa kiitikadi na shakhsia wenye taathira katika jamii.
Taarifa ya pamoja ya mashirika hayo likiwemo Amnesty International na Human Rights Watch imeelezwa kusikitishwa kwake na kuendelea ukandamizaji dhidi ya wanaharakati nchini Saudia.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kuwa, kuna haja ya kufanyika juhudi za kuhitimishwa ukandamizaji huo ambao kimsingi unakinzana waziwazi na haki za binadamu.
Aidha taarifa hiyo imemtaka Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia ambaye kimsingi kwa sasa ndiye mtawala wa nchi hiyo kuhitimisha ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya raia.
Hivi karibuni, Kamati ya Kutetea Haki za Binadamu Bara Arabu ilieleza katika taarifa kwamba inafanya uchunguzi kuhusu hali mbaya na hatari ya kibinadamu na ya haki za binadamu inayotawala nchini Saudi Arabia baada ya kuongezeka hukumu za kifo zinazotolewa na Mahakama ya Jinai ya Riyadh dhidi ya raia wa nchi hiyo wakiwemo wafungwa wa kisiasa, wanaharakati na hata waandamanaji.
Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Saudia imevunja rekodi ya kunyonga watu. Hii ni katika hali ambayo, kuanzia mwaka 2013 hadi Oktoba mwaka jana jumla ya watu 1100 walinyongwa nchini Saudia huku zaidi ya matukio 990 ya unyongaji huo yakifanyika katika kipindi cha utawala wa Mfalme Salman bin Abdul-Aziz kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2015.