Baraza la Kijeshi la Mali limepiga marufuku shughuli zozote za mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanafadhiliwa kifedha na Ufaransa.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, Abdullah Maygan, Waziri Mkuu wa serikali ya mpito na ya kijeshi ya Mali, ametangaza kuwa: ni marufuku kwa mashirika yote yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini Mali, ambayo yanafadhiliwa na vitega uchumi vya Ufaransa na usaidizi wa kifedha au teknolojia wa nchi hiyo, yakiwemo mashirika yanayohusika na masuala ya kibinadamu kuendesha shughuli zao nchini humo.
Kabla ya hapo waziri wa mambo ya nje wa Mali, Abdallah Diop, alimwandikia barua Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kumueleza kwamba: Ufaransa imekiuka mara kadhaa anga ya nchi hiyo na imewapatia silaha nyingi magaidi wenye misimamo ya kufurutu mpaka.
Katika barua yake hiyo kwa rais wa Baraza la Usalama la UN Diop ameongezea kwa kusema: tangu Januari mwaka 2021 hadi sasa, ndege zisizo na rubani za Ufaransa, helikopta na ndege za kivita za nchi hiyo zimeingia kwenye anga ya Mali karibu mara 50 bila kibali cha serikali ya mpito.
Uhusiano kati ya Ufaransa na Mali umeharibika vibaya tangu jeshi lilipoingia madarakani katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi mwaka 2020.