Mashtaka rasmi ya Russia kwa Umoja wa Mataifa kuhusu maabara za silaha za kibiolojia za Marekani nchini Ukraine

Russia imepeleka malalamiko yake rasmi kwa Umoja wa Mataifa kuhusu kuwepo kwa maabara za silaha za kibiolojia za Marekani nchini Ukraine. Vasily Nebenzia, ​​mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, amethibitisha kwamba nchi yake imekusanya ushahidi wa kutosha kuhusu uwepo wa maabara ya silaha hizo za kibiolojia za Marekani huko Ukraine.

Kwa kutuma barua mbili tofauti kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Baraza la Usalama la umoja huo, Nebenzia amesema: “Kwa mujibu wa kifungu cha sita cha Mkataba wa Kuzuia Kuenezwa Silaha za Kibiolojia na za Sumu, Moscow imetuma rasmi malalamiko yake kwa Baraza la Usalama ambapo imeyaambatanisha na ushahidi uliopo wa kuaminika kuhusu suala hilo.” Russia kwa mara nyingine tena imeomba kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kifanyike mara moja ili kuchunguza suala hilo.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 6 cha Mkataba wa Kuzuia Silaha za Kibiolojia na za Sumu, “nchi yoyote mwanachama wa mkataba huo inapogundua kuwa mwanachama mwingine anaenda kinyume na majukumu na masharti ya mkataba huo, inaweza kupeleka malalamiko yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.”

Jenerali Igor Krylov, Kamanda wa Vikosi vya Ulinzi wa Nyuklia, Kemikali na Kibiolojia wa Majeshi ya Russia, hapo awali alisema kwamba kuna mtandao wa maabara zaidi ya 30 za kibiolojia zinazojishughulisha na utengeneza wa silaha za maangamizi ya umati nchini Ukraine, ambazo hufanya kazi kwa maslahi ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon). Jenerali huyo wa Russia amesisitiza kwamba kila hatua imechukuliwa kwa ajili ya kuendeleza mipango ya kibiolojia ya kijeshi ya Marekani huko Ukraine baada ya kuanza operesheni maalum za kijeshi za Russia nchini humo.

Kufichuliwa kwa hatua za Marekani za kusaidia Ukraine katika uwanja wa kutengeneza silaha za kibiolojia kunaonyesha malengo halisi na ya kinyama ya Washington katika uwanja wa utengenezaji wa silaha mbalimbali za kibiolojia katika nchi hiyo kwa kisingizio cha eti ushirikiano wa kiulinzi kati ya Marekani na Ukraine. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imedai kuwa haina maabara zozote nchini Ukraine, katika hali ambayo ushahidi uliopo unaonyesha wazi kuwa Pentagon inasimamia moja kwa moja maabara hizo na kuwalipa mishahara wanakandarasi na wataalamu  wanaohudumu kwenye maabara hizo za utengenezaji wa silaha za kibiolojia.

Baada ya kusambaratika Umoja wa Kisiovieti, Washington ililipa kipaumbele maalum suala la kuanzisha maabara za silaha za kibiolojia katika nchi ambazo ziliundwa baada ya kuanguka umoja huo. Licha ya kwamba Marekani ni mwanachama wa “Mkataba wa Kuzuia Silaha za Kibiolojia” ulioidhinishwa mwaka 1972 na kuanza kutekelezwa mwaka 1975, lakini kwa kweli inachukuliwa kuwa moja ya waanzilishi na watengenezaji wakuu wa silaha hizo za maangamizi ya umati na zisizo za kibinadamu. Na hasa ikitiliwa maanani kwamba silaha hizo zinatengenezwa katika maabara zilizo kwenye nchi zilizo karibu na mpaka wa Russia kama vile Ukrainia, na hivyo kuwa tishio kubwa kwa usalama wa nchi hiyo. Rais Vladimir Putin wa Russia alionya Jumatano kuhusu nchi za Magharibi kuitumia Ukraine kama uwanja wa majaribio ya silaha za kibiolojia na kemikali.

Katika ujumbe wake wa televisheni kuhusu vita vya Ukraine, Putin alisema: “Utawala wa Kyiv umebadilika kuwa chombo cha sera za nje za Marekani na umepoteza mamlaka yake. Ardhi ya Ukraine pia imekuwa uwanja wa majaribio ya ya silaha za kibiolojia, na nchi hii sasa imekuwa ghala kubwa la silaha.”

Sisitizo la kiongozi wa ngazi ya juu zaidi wa Russia kuhusu kutumiwa Ukraine kama uwanja wa majaribio ya silaha za kibiolojia za Marekani linaonyesha wazi kuwa kwa mtazamo wa Moscow suala hilo lina umuhimu mkubwa na ni tishio kubwa kwa Russia. Kwa hivyo, inatarajiwa kwamba Russia baada ya kuwasilisha rasmi malalamiko yake katika Umoja wa Mataifa itafuatilia kwa umakini suala hilo ili kuthibitisha hatua ya Marekani kushirikiana na Ukraine katika kukiuka “Mkataba wa Kuzuia Usambazaji wa Silaha za Kibiolojia.”

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *