Mataifa ya Afrika kuharakisha utumiaji wa vitambulisho vya kidijitali

Mataifa ya Afrika jana Jumanne yalianza mkutano wa siku tatu katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi kujadili njia za kuharakisha utumiaji wa vitambulisho vya taifa vya kidijitali ili kuimarisha utoaji wa huduma za serikali.

Mkutano Mkuu wa 7 wa ID4Africa Augmented General (AGM) umezileta pamoja serikali, washirika wa maendeleo na wabunifu katika mkuktano huo wa Nairobi ili kutathmini jinsi utambulisho wa kidijitali unavyoweza kusaidia katika masuala ya usalama na kulinda heshima za watu na kurahisisha huduma kwa raia.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Julius Bitok, Katibu Mkuu katika Idara ya Taifa ya Uhamiaji na Huduma kwa Raia nchini Kenya, amesema kuwa, Kenya kwa sasa iko katikati ya mchakato wa kubadilisha vitambulisho vya taifa vya kidijitali kutoka kitambulisho cha kizazi cha pili hadi cha tatu.

Bitok alisema pia hiyo jana Jumanne kuwa, mfumo unaotegemewa katika vitambulisho hivyo vipya vya kidijitali utaipa serikali takwimu za kuaminika na kuisaidia sana kuwafikisha wananchi huduma kwa urahisi zaidi.

Wajumbe kutoka nchi 50 za Afrika wanashiriki kwenye kongamano hilo ili kuharakisha uchukuaji wa vitambulisho vya kielektroniki vitakavyowawezesha wananchi kupata huduma za elimu, afya na usalama wa jamii, kwa urahisi zaidi.

Kenneth Attafuah, katibu mtendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Kitaifa ya Ghana, naye amesema kwenye mkutano huo kwamba, Ghana tayari imezindua kitambulisho cha kidijitali ambacho hutolewa kwa raia wake pamoja na wakaazi wa kigeni waliotimiza masharti yanayotakiwa huko Ghana.

Attafuah ameongeza kuwa, kadi ya kidijitali ya Ghana ambayo imepachikwa chipu ya kibayometriki ina faida kubwa kwa sababu inathibitisha kwa wakati halisi utambulisho watu binafsi wanaotaka kupata huduma za umma.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *