Matamshi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu; Marekani imehusika katika machafuko nchini Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu jana Jumatano siku mbili kabla ya maadhimisho ya tarehe 13 Aban (4 Novemba 1978) ambayo hapa nchini ni Siku ya Taifa ya Kupambana na Ubeberu wa Kimataifa, alihutubia kikao cha mamia ya wanafunzi, akiitaja siku hiyo kuwa ni kielelezo cha uovu, ukhabithi na dhihirisho la kupata pigo na kushindwa Marekani.

Tarehe 13 Aban 1358 Hijria Shamsia (4 Novemba) inakumbusha matukio muhimu katika historia ya Iran. Kupelekwa uhamishoni Imam Ruhullah Khomeini nchini Uturuki tarehe 4 Novemba 1964, mauaji ya wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Tehran mnamo Novemba 4, 1978, na kutekwa kwa Pango la Ujasusi la Marekani (uliokuwa ubalozi wa Marekani mjini Tehran) mnamo Novemba 4, 1979 yalikuwa matukio matatu tofauti, ambayo kila moja lilikuwa na nafasi maalumu katika kuundika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu. Utambulisho wa matukio yote matatu ni mapambano dhidi ya ubeberu na mawakala na vibara wake, na kwa sababu hiyo, siku hii imepewa jina la “Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Ubeberu”.

Katika hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei ameitaja tarehe 13 Aban (4 Novemba) kuwa ni siku ya kihistoria na yenye ibra na  mafunzo. Ameashiria tukio la kupelekwa uhamishoni Imam Ruhullah Khomeini, mauaji ya idadi kubwa ya wanafunzi mbele ya Chuo Kikuu cha Tehran na shambulio la wanafunzi kwenye Ubalozi wa Marekani tarehe 4 Novemba 1979, na kusema: “Wamarekani na wenye mielekeo ya Kimarekani wana hasira na ghadhabu kuhusu siku hii muhimu na mikusanyiko yake inayojenga umoja; kwa sababu siku hii ni kielelezo cha maovu ya Marekani na uthibitisho wa udhaifu na uwezekano wa kushindwa kwake.”

Tunapotupia jicho kisa cha kupelekwa uhamishoni Imam Khomeini (RA) katika historia ya zama hizi ya Iran, tunaona kwamba hatua hiyo ilikuwa matokeo ya upinzani mkali wa Imam dhidi ya sheria iliyowapa washauri wa kijeshi wa Marekani nchini kinga ya kutofikishwa mahakamani iwapo wangepatikana na hatia ya aina yoyote (Capitulation Accord). Hatua hii ya Imam Khomeini kwa hakika, ilikuwa chanzo cha mapambano dhidi ya ubeberu na ukoloni hapa nchini. Sheria hiyo ilitambuliwa kuwa dharau kwa taifa la Iran na kwa msingi huo hayati Imam Ruhullah Khomeini siku kadhaa baada ya kupasishwa sheria hiyo bungeni alitoa hotuba ya kihistoria akieleza taathira zake na kumshambulia vikali Shah na Marekani. Baada ya hotuba hiyo Imam Khomeini alikamatwa na kupelekwa uhamishoni nje ya nchi. Kuuliwa shahidi wanafunzi Novemba 4, 1978, baada ya wanafunzi kwenda katika Chuo Kikuu cha Tehran kupinga utawala wa Shah, na kutekwa Pango la Ujasusi (ubalozi wa Marekani mjini Tehran), ambako kwa mujibu wa Imam Khomeini, yalikuwa mapinduzi ya pili, ni mwendelezo wa vuguvugu la mapinduzi ya wananchi dhidi ya ubeberu na mabeberu.

Ubalozi wa Marekani nchini Iran ulikuwa sehemu ya kutoa taarifa za siri kwa serikali ya Washington. Baadhi ya nyaraka zilizogunduliwa baada ya kutekwa eneo hilo zinaonyesha kuwa Marekani ilikuwa inapanga kufanya njama dhidi ya Iran na ilikuwa ikipinga ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Baada ya kutekwa pango hilo la ujasusi, serikali ya rais wa wakati huo wa Marekani, Jimmy Carter, ilizuia mali na maslahi yote ya Iran nchini humo tarehe 8 Novemba 1979 kwa kisingizio kwamba Iran ni tishio kwa usalama wa taifa la Marekani. Siasa hii ya Marekani ya kuiwekea mashinikizo Iran ingali inaendelea kwa njia zote za kisiasa, kiuchumi na hata kijeshi tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia kuhusika kwa Marekani katika machafuko ya wiki chache zilizopita nchini Iran na kusema: “Taarifa ya pamoja la Wizara ya Usalama wa Ndani na Shirika la Upelelezi la Jeshi la Walinzi waMapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kuhusu machafuko hayo imekusanya habari na uvumbuzi muhimu na inaonyesha kuwa adui alikuwa amepanga njama kwa ajili ya Tehran na miji mikubwa na midogo hapa nchini.”

Kama alivyosema Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, nyaraka za kijasusi zinaonyesha kuwa, Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kwa ushirikiano na mashirika ya ujasusi ya washirika na vibaraka wake, walipanga kuzusha machafuko na pia kutayarisha uwanja wa kuzidishwa mashinikizo ya kigeni dhidi ya Iran. Taarifa za kiintelijensia zinaonesha kuwa, CIA imekuwa na ushirikiano wa karibu na Idara ya Ujasusi wa Kigeni ya Uingereza (MI6), shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel (MOSSAD), Idara ya Ujasusi wa Kigeni wa Saudia na nchi nyingine kadhaa katika kutekeleza mpango huo.

Ushahidi na tajiriba ya kihistoria vinaonyesha kuwa serikali ya Marekani imekuwa mojawapo ya waungaji mkono wakuu wa machafuko na ghasia za mitaani nchini Iran katika miongo kadhaa iliyopita na kwa uchache katika miaka ya hivi karibuni. Matukio na machafuko ya wiki chache zilizopita nchini Iran pia yanaonesha kuwa, maadui ikiwemo Marekani, wanatumia masuala kama vile haki za binadamu na haki za wanawake kama fursa ya kuibua machafuko, mifarakano na kuzusha migawanyiko katika jamii ya Iran na wamewekeza tangu hapo kabla kwa ajili ya njama hiyo. Taarifa ya hivi karibuni ya mashirika ya ujasusi ya Iran pia imesema kuwa idara za kijasusi za Magharibi na Kizayuni zinatoa kozi za mafunzo ya pamoja ya wakufunzi wa “vita mseto” (Hybrid warfare) kwa idadi kubwa ya vibaraka wao ambao wamewapa jukumu la kuhamisha mafunzo hayo kwa wengine na kisha kuyatekeleza kivitendo.

Uwanja mwingine mkuu wa harakati za idara za ujasusi za adui kwa ajili ya kuzusha au kuchochea machafuko nchini Iran ni kijaribu kuathiri matabaka tofauti kama vile walimu, wafanyakazi na wanafunzi wa vyuo vikuu kwa kuunda makundi bandia na maovu na kuongoza au kuelekeza harakati za kuyatumia vibaya matabaka hayo.

Katika hotuba yake mbele ya mkusanyiko wa wanafunzi, Ayatullah Ali Khamenei pia ameashiria uongo mkubwa wa Wamarekani kwamba eti wanalionea huruma taifa la Iran na kusisitiza kuwa: “Katika vita mseto vya wiki chache zilizopita, Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, baadhi ya madola ya Ulaya na makundi washirika yametumia rasilimali zao zote kwa ajili ya kutoa pigo dhidi ya taifa la Irani, lakini taifa limetoa dhoruba kali kwa wasiolitakia mema na kutibua mipango yao.”

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *